Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

26 Juni 2023

13:26:52
1375552

Onyo la Umoja wa Mataifa kuhusu kuongezeka duniani dawa za kulevya za viwandani

Umoja wa Mataifa umeonya juu ya "matokeo ya maafa" ya kuongezeka kwa kasi dawa za kulevya za viwandani katika ngazi za kimataifa.

Kupitia taarifa iliyochapishwa Jumapili na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu sambamba na ripoti yake ya kila mwaka, ofisi hiyo inasema kwamba Fentanyl, dawa ya viwandani ambayo ina nguvu mara 50 zaidi ya heroin, imebadilisha kwa kiasi kikubwa matumizi ya dawa za kulevya huko Amerika Kaskazini.

Ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeonya kuhusu "matokeo ya maafa" ya hali hiyo na kuongeza kwamba "uzalishaji wa bei nafuu, wa haraka na rahisi" wa dawa za kulevya za viwandani umeibua masoko mengi duniani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na dawa za Kulevya na Uhalifu, katika mwaka 2021, vifo vingi vilisababishwa na utumiaji wa kupindukia wa dawa za kulevya katika eneo hilio na kwamba kuna uwezekano wa kuongezeka ulimwenguni uzalishaji wa dawa hizo hatari.

Shirika hilo la kimataifa limeonya kwamba kwa kutilia maanani taaluma inayotumika katika uzalishaji wa dawa hizo za viwandani na masoko yanayoibuka kila uchao katika eneo hilo la Amerika Kaskazini, ulanguzi wa dawa hizo utaongezeka maradufu katika eneo hilo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu pia imeashiria hali ya Afghanistan na kusema: Matarajio ya kupungua kilimo cha mipopi kutokana na marufuku inayotekelezwa na serikali ya Taliban dhidi ya kilimo hicho kinachotumika katika utengenezaji wa dawa za kulevya huenda yakaleta mabadiliko katika mwelekeo wa uzalishaji wa mada ya methamphetamine.

Kwa sasa Afghanistan ni mojawapo ya wazalishaji wakuu wa mada hiyo ya kulevya ambayo inazalishwa kinyume cha sheria.

Mkurugenzi mtendaji wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa kwamba jamii ya kimataifa inapasa kuongeza juhudi za kupambana na magenge ya walanguzi wa dawa za kulevya ambao wanatumia vibaya mapigano na migogoro ya kimataifa ili kupanua uzalishaji wa dawa za kulevya hasa za viwandani.

Ripoti hiyo pia inaonya kuhusu athari hasi za kimazingira na kiuchumi za dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, watu milioni 296 waliripotiwa kutumia dawa za kulevya mwaka 2021, ambalo ni ongezeko la asilimia 23 katika kipindi cha miaka 10.

342/