Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

26 Juni 2023

13:31:08
1375559

Wanaharakati walaumu sera za uhamiaji za Ulaya kwa vifo vya wahajiri

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wamekosoa sera za uhamiaji za Ulaya, huku vifo vya wahajiri wanaosafiri kwenda Ulaya hasa kupitia baharini vikiongezeka.

Jukwaa la Kijamii la Wahajiri la Magharib (FSMM) lilitoa taarifa ya kulaani sera hizo mbovu za Wamagharibi jana Jumapili, katika mkusanyiko wa wanaharakati wa kutetea haki za wahajiri katika mji wa Nador, kaskazini mashariki mwa Morocco.

Wanaharakati hao walikusanyika kwa ajili ya kuwakumbuka wahajiri 23 wa Kiafrika walioaga dunia mwaka jana wakati kama huu, katika mkanyagano wa kujaribu kuingia katika mji wa Melilla unaodhibitiwa na Uhispania kaskazini mwa Morocco.

Baadhi ya duru za habari zilisema walioaga dunia katika tukio hilo ni wahajiri 37, waliposhambulia na askari wa Uhisnapnia wakijaribu kuruka uzio wa chuma unaoyatenganisha maeneo hayo mawili, huko kaskazini mwa Morocco.

Jukwaa hilo linajumuisha wanahakati wa haki za binadamu kutoka Morocco, Algeria, Tunisia na Libya, Asasi Zisizo za Kiserikali za Kimataifa na jumuiya za wahajiri wa Kiafrika kutoka Uhispania, Ufaransa, Ubelgiji na Morocco.

Aidha haya yanajiri siku chache baada ya kuzama mashua ya wahamiaji kwenye Rasi ya Mora ya Ugiriki, na kusababisha vifo vya watu 81 na wengine 500 kutoweka. Ni wahajiri 104 pekee waliokolewa mpaka sasa katika janga hilo kwenye Bahari ya Mediterraenia.

Hivi karibuni pia, Nasser Kan’ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema Magharibi inajaribu kukwepa kubeba dhima ya mgogoro wa wakimbizi unaoshuhudiwa hivi sasa duniani, na kwamba sera mbovu za Marekani na nchi za Ulaya ndizo zinazofaa kulaumiwa kwa mgogoro huo.

342/