Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

29 Juni 2023

14:45:51
1376053

Vikwazo ni sawa na silaha ya kivita

Katibu wa Kamati ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama ya Iran amesema kuwa, vikwazo ni jinai kubwa dhidi ya binadamu na kwamba Marekani ndiye mtendaji mkuu wa jinai hiyo kutokana na uraibu wake wa kuziwekea vikwazo nchi nyingine bila ya sababu ya maana.

Kazem Gharib Abadi amesema hayo na kuongeza kuwa, Marekani hivi sasa imeziwekea vikwazo vya upande mmoja nchi karibu 25 duniani. Amesema, vikwazo vya kidhulma na haramu vya Mrekani dhidi ya wananchi wa Iran ndiyo jinai kubwa zaidi inayoendelea kufanywa hivi sasa na dola hilo la kiistikbari.

Katika miongo ya hivi karibuni, vikwazo vya kiuchumi ndiyo silaha kuu ambayo imekuwa ikitumiwa na madola ya kibeberru ya Magharibi dhidi ya nchi nyingine duniani. Hadi hivi sasa Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zimeziwekea nchi nyingine vikwazo kwa mamia ya mara na hizo ni katika jinai kubwa dhidi ya binadamu duniani. 

Mara nyingi vikwazo hivyo vimekuwa vikiwekwa kwa visingizio kama vya kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia na eti kupigania haki za binadamu. Lakini ukweli ni kwamba daima vikwazo hivyo vina malengo ya kisiasa na shabaha yake kuu ni kuendeleza siasa za kibeberu za madola hayo.  

Katika siasa za mambo ya nje za Marekani, suala la vikwazo vya kiuchumi ni katika silaha kubwa zinazotumiwa kuzishinikiza nchi na makundi mengine ambayo hayakubali kuburuzwa na dola hilo la kibeberu. Marais wote wanaoingia madarakani nchini Marekani wanaipa umuhimu mkubwa silaha hiyo na ndio maana hata wasomi wengi duniani wamo kwenye orodha ya vikwazo vya kiuchumi vya dola hilo la kiistikbari.

Thomas Woodrow Wilson, rais wa 28 wa Marekani alisema: Taifa ambalo limewekewa vikwazo, hulazimika kusalimu amri au kuzingirwa kila upande; itumieni silaha hiyo ya kiuchumi isiyo ya umwagaji wa damu lakini angamizi na hakuna haja ya kutuma jeshi.

Hii ni katika hali ambayo, athari mbaya za vikwazo hivyo dhidi ya watu wa kawaida wa nchi husika ni kubwa. Vikwazo vinapotumiwa kama silaha ya kiuchumi vinaweza kuwa na athari mbaya na haribifu kuliko hata vita vya kijeshi. 

Bo Ram Kwon, mtaalamu na mtafiti Mmarekani anasema: Huko nyuma baadhi ya nchi zilikuwa zinatumia nguvu za kijeshi na pia vikwazo vya kiuchumi kama njia ya kuzishinikiza nchi nyingine.

Vikwazo vinaweza kusababisha hasara kubwa kwa nchi bila ya kuonekana damu ikimwagika hadharani na bila ya kuchochea hisia na malalamiko ya walimwengu, hivyo tunaweza kusema kuwa, silaha hiyo inapandelewa zaidi na wawekaji wa vikwazo kwa ajili ya kuyashinikiza mataifa mengine. 

Watafiti wengine wawili wa masuala ya kiuchumi wanaojulikana kwa majina ya Matthias na Florian wamesema kuwa, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi mbalimbali duniani vimethibitisha kuwa vimeleta ukosefu wa uadilifu, vimeongeza umaskini na kupunguza kiwango cha uzalishaji wa ndani wa nchi hizo. Kwa mfano vikwazo vya Mrekani vya baina ya miaka ya 1991 na 2018 vimesababisha karibu asilimia 3.5 ya umaskini katika nchi mbalimbali duniani. Wastani wa uzalishaji wa mali ghafi katika nchi zilizowekewa vikwazo hivyo nao umepungua kwa zaidi ya asilimia 2.

Tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko chini ya vikwazo vya kila namna vya Marekani ambayo katika miaka ya hivi karibuni vikwazo hivyo vimeongezeka sana kiasi kwamba biashara za nchi zimeathirika na sehemu ya vyanzo vya mali vya Iran vimetoweka au vimesimamishwa, masuala ambayo yanapelekea kuongezeka umaskini, mfumuko wa bei na mashinikizo kwa wananchi.

Miongoni mwa athari mbaya za vikwazo hivyo ni taarithira zake za moja kwa moja kwa usalama wa kiafya wa wananchi wa Iran na huo ni uvunjaji wa wazi kabisa wa haki za binadamu. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hata wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa, vikwazo haramu vya Marekani vinaathiri moja kwa moja usalama wa kiafya wa wananchi wa Iran wakiwemo wale wenye magonjwa yaliyo vigumu kutibika. Vikwazo hivyo vinasababisha watu wenye magonjwa magumu kutibika, kupoteza maisha yao kila siku nchini Iran. Hivyo lazima tuseme kuwa, vikwazo ni sawa na silaha ya kivita ambayo uharibifu wake unashuhudiwa katika kona na pande mbalimbali. 

342/