Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

1 Julai 2023

20:17:35
1376415

Marekani yatetea kuchomwa moto Qurani Sweden, UN yalaani

Huku ulimwengu wa Kiislamu ukiendelea kulaani vikali kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu huko nchini Sweden, Marekani imetoa taarifa inayoonekana kuunga mkono na kuhalalisha kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu.


Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amedai kuwa, kitendo cha kuchomwa moto Qurani Tukufu Sweden kimefanyika kutokana na uhuru wa maoni na kujieleza, na eti uhuru huo ni msingi wa demokrasia.

Miller ameendelea kuropoka na kujikanganya kwa kusema, "Tunaamini kuwa watu wa haki ya kufanya vitendo hivyo (vya kuchoma moto Qurani), lakini pia vitendo hivyo havifai."

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa US ameongeza kuwa: Tunatiwa wasiwasi na kitendo hicho, lakini tunaunga mkono uhuru wa kujieleza na uhuru wa watu kukusanyika, kama misingi ya demokrasia.

Huku hayo yakiarifiwa, Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ya kulaani kudhalilishwa kwa maandishi matakatifu ya Kiislamu nchini Sweden na kusema kuwa, vitendo vya aina hiyo vinapasa kukosolewa vikali.

Kamishna Mkuu wa Jumuiya ya Ustaarabu ya Umoja wa Mataifa (UNAOC), Miguel Moratinos amesema kuwa, kitendo hicho cha kuchomwa moto Qurani ni sumu ya chuki na kuwavunjia heshima Waislamu wakisherehekea sikukuu za Iddul Adh'ha.

Afisa huyo wa UN amesisitiza kuwa, "Katika hali ambayo uhuru wa kujieleza una umuhimu mkubwa, lakini watu kuheshimiana kwa shabaha ya kuhamasisha amani katika jamii kwa misingi ya haki za binadamu na heshima kwa wote, kuna umuhimu mkubwa zaidi pia."