Main Title

source : Parstoday
Jumanne

4 Julai 2023

20:27:31
1377176

Uturuki na Misri zateua mabalozi na kurejesha kikamilifu uhusiano wao wa kidiplomasia

Uturuki na Misri zimeteua mabalozi wa pande mbili ili kurejesha rasmi uhusiano wao katika ngazi ya juu ya kidiplomasia.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na wizara ya mambo ya nje ya Uturuki, Cairo na Ankara zimesema, Uturuki imemteua Salih Mutlu Sen kuwa balozi wake mjini Cairo na Misri kwa upande wake imemteua Amr Elhamamy kuwa balozi wake mjini Ankara.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, kuinua kiwango cha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kumetekelezwa kwa mujibu wa uamuzi uliochukuliwa na marais wa nchi mbili.

Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: hatua hiyo inalenga kurekebisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na inaonyesha nia ya pande zote ya kuboresha uhusiano wa nchi mbili kwa maslahi ya watu wa Uturuki na Misri.

Uturuki na Misri, ambazo ni washindani wa kikanda, zimekabiliana katika nyanja nyingi za kieneo huku viongozi wao wakishambuliana kwa matusi hadharani. Hata hivyo kuanzia mwaka 2020 ziliingia katika mchakato wa kuwa na uhusiano wa karibu.

Katika mwaka huu wa 2023 pia, Ankara na Cairo zimeshiriki katika duru kadhaa za mazungumzo kwenye ngazi ya mawaziri sambamba na kutumiana jumbe za kirafiki na kujadiliana kwa uwazi juu ya kuanzisha tena uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Juhudi za maelewano kati ya Uturuki na Misri zilichukua mkondo muhimu baada ya Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan kupeana mikono kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar mwishoni mwa mwaka 2022.../

342/