Main Title

source : Parstoday
Jumatano

5 Julai 2023

17:59:51
1377421

Vifo vya uzazi Marekani vimongezeka kwa asilimia 100, waathirika wakuu ni Wamarekani Waafrika

Vifo vya uzazi kote Marekani vimeongezeka zaidi ya mara mbili katika miongo miwili iliyopita, huku wanawake wenye asili ya Afrika au Wamarekani weusi wakifariki kwa kiwango cha juu zaidi, utafiti mpya umefichua.

Kulingana na utafiti uliochapishwa Jumatatu katika Jarida la Jumuiya ya Madaktari ya Marekani, akina mama wenye asili ya Afrika walikufa kwa viwango vya juu zaidi katika taifa hilo, huku ongezeko kubwa zaidi la vifo likiwa miongoni  mwa akina mama wa jamii za asili za nchi hiyo za Wamarekani Wahindi na wenyeji wa Alaska,

Ripoti hiyo imebainisha kuwa makundi ya wachache kwa mtazamo wa rangi na kabila yanazidi kukumbwa na  hali mbaya zaidi kuliko makundi mengine. Kwa ujumla Wazungu wa Marekani ndio wanaonekana kuwa na hali bora zaidi.

Watafiti wanaofanya utafiti huo waliangalia vifo vya uzazi kati ya 1999 na 2019 kwa kila jimbo na makabila matano.

Dk. Allison Bryant, mmoja wa watafiti hao amesema ripoti hiyo inaonyesha kuwepo ubaguzi wa rangi katika sekta ya tiba.

Kulingana na ripoti hiyo, ikiwa miongoni mwa mataifa tajiri zaidi duniani, Marekani ina kiwango cha juu zaidi cha vifo vya uzazi.

Utafiti huo umebaini kuwa wanawake Wamarekani wenye asili ya Afrika walikuwa na kiwango kikubwa cha wastani cha vifo vya uzazi kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwa wakiwa hai, ambacho kiliongezeka mara tatu katika baadhi ya majimbo ya kaskazini mashariki kwa miongo miwil.

Katika jimbo la Arkansas, wanawake weusi wana uwezekano maradufu wa kufariki kwa sababu zinazohusiana na ujauzito ikilinganishwa na wanawake wazungu, kulingana na ripoti ya serikali ya 2021.

Dk. William Greenfield, daktari mkuu anayesimamia ustawi wa familia katika Idara ya Afya ya Arkansas, amesema kuwa tofauti hiyo ni kubwa na "imedumu" kwa miaka mingi. Pia ameongeza kuwa ni changamoto kubainisha kwa usahihi sababu za kuongezeka kiwango cha vifo vya uzazi kwa akina mama weusi katika jimbo hilo.

Waandishi wa ripoti hiyo pia wamesisitiza umuhimu wa kufahamu tofauti hizo ili kujikita katika suluhu ambazo zimekita mizizi katika jamii na kubaini rasilimali muhimu za kushughulikia suala hilo.