Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

8 Julai 2023

20:22:19
1377984

NATO kuanzisha maeneo matatu ya kiulinzi kwa lengo la kukabiliana na Russia

Katibu Mkuu wa shirika la kijeshi la NATO ametangaza kuwa katika mkutano utakaofanyika wiki ijayo, shirika hilo litaidhinisha mpango wa kuanzisha maeneo matatu ya kiulinzi Kaskazini (Bahari ya Atlantiki na Aktiki), Kituo cha (eneo la Balkan na Ulaya ya Kati) na Kusini (ya Bahari Nyeusi na Mediterania).

Jens Stoltenberg amesema madhumuni ya kuanzisha maeneo hayo matatu ya ulinzi ni kuboresha na kuimarisha uwezo wa kuzuia hujuma wa nchi wanachama wa NATO dhidi ya tishio la ugaidi na Russia. Stoltenberg amezungumzia pia kuongezeka kwa asilimia 8.3 matumizi ya kiulinzi ya shirika hilo la kijeshi katika mwaka huu 2023 na kueleza kwamba: NATO inaandaa msaada mwingine wa kijeshi wenye thamani ya yuro milioni 500 ili kukidhi mahitaji muhimu ya Ukraine kama vile mafuta, vipuri na mahitaji ya matibabu. Katibu Mkuu wa NATO ameongeza kuwa, ajenda nyingine muhimu zaidi itakayojadiliwa katika mkutano wa wiki ijayo wa wakuu wa nchi wanachama ni njia za kuiwezesha Ukraine kuwa mwanachama wa shirika hilo la kijeshi.

 

Mkutano wa NATO umepangwa kufanyika Vilnius, mji mkuu wa Lithuania, tarehe 11 na 12 za mwezi huu wa Julai. Kujipanua NATO kuelekea Mashariki na kuwepo muungano huo wa kijeshi wa Magharibi nchini Ukraine na baadhi ya jamhuri za uliokuwa Umoja wa Kisovieti wa Urusi ni miongoni mwa mambo yaliyoitia wasiwasi Russia. Moscow imeionya NATO mara kadhaa kuhusu hatua ya kuzipatia uanachama jamhuri za zamani za lililokuwa shirikisho la Kisovieti la Urusi katika shirika hilo la kijeshi na kusisitiza kuwa kufanya hivyo ni tishio kwa usalama wake wa taifa. Kuzuia Ukraine isigeuzwe kuwa kambi ya kijeshi ya NATO, ni moja ya sababu ambazo Russia inasema zimeifanya ianzishe operesheni za kijeshi ndani ya ardhi ya nchi hiyo.../