Main Title

source : Parstoday
Jumapili

9 Julai 2023

20:09:09
1378281

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi yaanza tena Ufaransa, askari polisi waingilia kati

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi ya Ufaransa yalianza tena jana nchini humo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kila mwaka ya mauaji ya Adama Traoré, raia mweusi ambaye ni miongoni mwa waathirika wa ukatili wa polisi nchini Ufaransa.

Adama Traoré aliuawa 2016 katika mazingira sawa na yale ya mauaji ya George Floyd huko Marekani kutokana na ukatili wa kutisha wa polisi ya Ufaransa.

Idadi kubwa ya watu wa Ufaransa walikusanyika jana katika viwanja vya Paris kufuatia mwito wa kuadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya Adama Traore na kupinga ukatili wa vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Licha ya upinzani mkubwa wa serikali ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, maandamano hayo yalianza kutoka Place de la République katikati mwa Paris kwa kaulimbiu ya "kulaani ukatili wa polisi."

Huku wakitangaza kuchukizwa na kukasirishwa na ukatili  wa kupindukia wa polisi wa Ufaransa, waandamanaji hao walishutumu tabia na mienendo ya kibaguzii ya polisi wa nchi hiyo.

Murielle Guilbert, mwakilishi mkuu wa vyama vya wafanyakazi vya Ufaransa vinavyojulikana kama Syndicale Solidaires, ameishutumu serikali kwa "kukanusha kuwepo kwa ukatili wa polisi" na "ubaguzi wa rangi".

Kiongozi wa chama chenye siasa kali za mrengo wa kushoto "Ufaransa Haitasalimu Amri" pia amekosoa vikali sera za serikali ya Macron za kukandamiza maandamano ya hivi majuzi nchini humo.

Jumanne ya tarehe 27 ya mwezi uliopita, afisa mmoja wa jeshi la polisi la Ufaransa alimuua kwa kumpiga risasi kijana aliyekuwa na umri wa miaka 17 mwenye asili ya kaskazini mwa Afrika, Nahel Merzouk. Ukatili huo wa mchana kweupe umezusha maandamano makubwa yaliyoendelea kwa siku kadhaa katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

342/