Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

10 Julai 2023

16:12:07
1378525

Mzigo mzito wa gharama za kiuchumi ambao serikali ya Erdogan inawabebesha Waturuki

Serikali ya Recep Tayyip Erdoğan imeongeza kodi inazowatoza wananchi wa Uturuki ili kuongeza mapato yake sambamba na kukabiliana na hali mbaya ya uchumi inayoikabili nchi hiyo.

Tovuti ya habari ya gazeti la Duvar imetoa ripoti kuhusiana na suala hilo na kuandika: "serikali ya Uturuki inapanga kukusanya mapato ya lira bilioni 30 zaidi kwa kuongeza kodi ya ongezeko la thamani." Mnamo tarehe 7 Julai, wananchi wa Uturuki walianza kukabiliana na wimbi jipya la ongezeko la kodi. Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) imeongezeka pia kwa asilimia mbili katika bidhaa na huduma, kutoka asilimia 18 hadi asilimia 20, huku kiwango cha kodi ya ongezeko la thamani cha asilimia nane kinachotumika kwa baadhi ya bidhaa kikiongezeka hadi asilimia 10. Viwango vipya vitatumika rasmi kuanzia tarehe 10 Julai.

Kwa upande mwingine, ongezeko hilo la kodi haliishii kwenye kodi ya ongezeko la thamani pekee. Kwa mujibu wa uamuzi uliochukuliwa na serikali, gharama za mazungumzo ya simu ya nje ya nchi imeongezeka kutoka lira 6019 hadi lira elfu 20, na ushuru wa benki kwa mikopo wanayopatiwa watu nao pia umeongezeka kutoka 10% hadi 15%. Na hii ni katika hali ambayo, gharama ya utoaji viza, ofisi za utoaji hati rasmi na paspoti imeongezeka kwa 50%. Hivi karibuni serikali ya Erdogan imeongeza maradufu ushuru wa magari ya usafiri (OTV) na ushuru wa kawaida wa mashirika kutoka 20% hadi 25%. Mtaalamu wa uchumi Oyak Yatirim  ametabiri kwa kusema: "Kuongezwa kodi ya kampuni  kutaipatia serikali mapato ya zaidi ya lira bilioni 100 na ushuru wa magari ya OTV utaipatia takriban lira bilioni 40  katika mwaka huu wa 2023".

Miezi miwili baada ya ushindi wa Recep Tayyip Erdogan wa kukalia kiti cha urais wa Uturuki kwa muhula wa tatu mtawalia, imedhihirika wazi kuwa Erdogan na serikali anayoiongoza hawajaweza kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais. Wakati wa hekaheka za uchaguzi uliofanyika hivi karibuni, Rais wa Uturuki aliwataka wananchi wamwamini na kuacha kuwapigia kura wapinzani. Erdoğan aliwataja wapinzani wa serikali yake kama vibaraka wanaopanga kuinasisha tena Uturuki kwenye mtego wa njama za Marekani na Magharibi.

Hii ni katika hali ambayo, wachambuzi wanaoipinga serikali ya Erdogan walikuwa wamesisitiza kuwa endapo kiongozi wa muungano wa upinzani Kemal Kılıçdaroğlu atashindwa katika uchaguzi itafika siku watu wa Uturuki watalazimika kununua hata vitunguu na mbatata kwa idadi na kushindwa kununua bidhaa hizo kwa kilo. Katika mkesha wa duru ya pili ya uchaguzi wa 13 wa rais nchini Uturuki, mwanauchumi mashuhuri wa Uturuki Ali Bayramoglu aliishauri timu ya wapinzani ya serikali ya Erdogan kwa kusema:

"Ikiwa mnataka mshinde, jitahidini kuhakikisha kuwa mnawaeleza wananchi kwa usahihi hali mbaya mno ya kiuchumi iliyonayo Uturuki." 

Ali Babajan, kiongozi wa chama Demokrasia na Maendeleo (DEVA) na mmoja wa wachumi wabobezi wa Uturuki, ambaye akiwa waziri wa uchumi, alitoa mchango mkubwa kwa uchumi wa Uturuki katika muongo wa kwanza wa serikali ya Erdogan, naye pia aliorodhesha hatari kadhaa ambazo zitatokea ikiwa Erdogan atachaguliwa tena ikiwemo kiwango cha njaa kuongezeka hadi lira 50,000.

Hivi sasa, mamilioni ya watu wa Uturuki wanaishi kwa dhiki kubwa kwa kutegemea kiwango cha ujira na mshahara wa lira 8,500. Babajan, alisisitiza pia wakati huo kwa kusema:

"Ikiwa Erdogan atashinda, kila mtu mmoja atakuwa masikini zaidi na nafasi na umuhimu wa Uturuki katika uchumi wa dunia utashuka."

Inavyoonekana, ukiwa umepita muda wa chini ya miezi miwili tangu yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Uturuki, utabiri uliofanywa na mrengo wa upinzani, hasa katika uga wa kiuchumi umeonekana kuwa makini na sahihi zaidi. Kwa miezi kadhaa sasa, wananchi wa Uturuki wanasokotana na makali ya kiuchumi, na kutokana na kuongezeka kwa bei, tutarajie kushuhudia upinzani na malalamiko ya watumiaji dhidi yaongezeko la bei. Ukweli ni kwamba Uturuki bado inakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan, licha ya ahadi zake za wakati wa kampeni za uchaguzi, hadi sasa hajaweza kupata mafanikio yoyote katika kutatua au kupunguza makali ya hali hiyo. Baada ya kushinda uchaguzi wa urais mwezi Mei na kushika tena hatamu za uongozi, Erdogan ameteua wapitishaji maamuzi wapya wa masuala ya fedha na uchumi. Lakini maamuzi ya timu hiyo mpya nayo pia hayajawa na matokeo chanya. Kuongezeka kwa riba ya benki ulikuwa uamuzi wa kwanza kuchukuliwa na serikali mpya ya Erdoğan, ambao haukuwa na tija yoyote.../

342/