Main Title

source : Parstoday
Jumanne

11 Julai 2023

19:32:38
1378843

Uswidi: Waislamu waandamana kulaani uchomaji wa Qur'ani Tukufu

Mamia ya Waislamu huko Uswidi wameandamana katika mji mkuu, Stockholm kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi hiyo ya Ulaya.

Mji mkuu wa Sweden ulishuhudia maandamano makubwa siku ya Jumapili, ambapo Waislamu waliandamana kupinga matukio ya hivi karibuni ya uchomaji moto Qur'ani Tukufu nchini humo.

Maandamano hayo yaliandaliwa na makundi ya Waislamu katika Medani ya Medborgarepaltsen mjini Stockholm, ambapo waandamanaji wapatao 500 walitoa wito wa kupigwa marufuku kisheria vitendo hivyo vya kutoheshimu kitabu kitakatifu cha Uislamu.

Waandaaji wamesema katika taarifa yao kuwa kuchoma moto Qur'ani Tukufu ni kitendo cha chuki dhidi ya Uislamu ambacho kinaumiza hisia za Waislamu na kwamba vitabu vitakatifu vinapaswa kulindwa ili visivunjiwe heshima.

Mikail Yuksel, kiongozi wa chama cha Nyans (Nnuance), aliliambia Shirika la Habari la Anadolu kwamba uchomaji wa Qur'ani Tukufu haukubaliki kisheria.

Alisema vitendo hivyo vinapaswa kuchukuliwa kuwa uhalifu wa chuki na kwamba havina nafasi katika jamii za kidemokrasia. Aliomba marekebisho ya kisheria yafanyike kuhusu suala hilo.

Mwezi uliopita, mtu mmoja alichoma nakala ya  Qur'ani Tukufu chini ya ulinzi wa polisi mbele ya Msikiti wa Stockholm.

Alichagua kufanya kitendo hicho kiovu katika siku kuu ya Eid al-Adha, mojawapo ya sherehe muhimu za Kiislamu zinazoadhimishwa na Waislamu duniani kote.

Kitendo chake kilizua hasira na kulaaniwa na nchi nyingi za Kiislamu, zikiwemo Iran, Uturuki, Saudi Arabia, Iraq, Pakistan, na Morocco.

Mnamo Januari, uchomaji mwingine wa Qur'ani Tukufu ulifanywa na mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia nje ya Ubalozi wa Uturuki nchini Uswidi.