Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

14 Julai 2023

09:57:17
1379295

Macron apokea zawadi ya kidole kilichokatwa kwenye kifurushi cha posta!

Chanzo cha usalama nchini Ufaransa kimetangaza kwamba kifurushi cha posta kilichokuwa na kidole kilichokatwa kimetumwa Ikulu ya Elysee na makazi ya Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron.

Gazeti la Ufaransa "Valeurs actuelles" limekinukuu chanzo cha usalama nchini huko kwamba, kifurushi hicho kilichokuwa na kidole kilichokatwa cha binadamu kilitumwa kwa njia ya posta Ikulu ya Elysee, makazi ya Rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron.

Chanzo hicho cha usalama kimefichua kuwa idara ya kupokea vifurushi katika Ikulu ya Elysée ilipokea kifurushi hicho baina ya tarehe 9 na 10 mwezi huu wa Julai, kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Ufaransa yanayofanyika leo, Julai 14.

Gazeti hilo la Ufaransa limeripoti kuwa kifurushi hicho hakikuwa na ujumbe wowote wa maandishi, na kilikuwa na kidole kilichokatwa tu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utambulisho wa mmiliki wa kidole hicho umetambuliwa. Baada ya kugundua utambulisho wa mtu huyu, maafisa wa Ufaransa walichukua hatua, ikiwa ni pamoja na huduma ya matibabu.

Ikulu ya Elysee imekataa kutoa maoni juu ya tukio hili, ambalo linaweza kutambuliwa kuwa aina ya vitisho au maandamano dhidi ya serikali.

Hivi karibuni Ufaransa imeshuhudia wimbi kubwa la maandamano yaliyositisha shughuli zote katika maeneo tofauti ya nchi hiyo baada ya kijana mmoja mwenye asili ya Afrika kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa nchi hiyo.

342/