Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

14 Julai 2023

09:58:20
1379298

Nchi masikini zinalipa riba mara 4 zaidi ya Marekani na mara 8 zaidi ya nchi tajiri za Ulaya

Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ya madeni duniani inayoonesha kuwa viwango vya deni la umma ni vya kushangaza na vinaongezeka; na viwango vya madeni yasiyo endelevu vinazidi kulimbikizika katika nchi masikini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ujumbe wa ripoti hiyo mwaka huu ni kuwa nusu ya dunia yetu inazama katika janga la maendeleo, linalochochewa na mzozo mkubwa wa madeni.

Amesema ripoti hiyo imebainisha watu bilioni 3.3 ambao ni karibu nusu ya wanadamu wote duniani wanaoishi katika nchi ambazo hutumia zaidi pesa zao kufanya malipo ya riba ya deni kuliko kuwekeza kwenye elimu au afya. Imeelezwa katika ripoti kuwa madeni ni nyenzo muhimu ya kifedha ambayo inaweza kuendesha maendeleo na kuwezesha serikali kulinda na kuwekeza kwa watu wao, lakini nchi zinapolazimika kukopa kwa ajili ya kujikimu kiuchumi, deni huwa mtego ambao huzalisha deni zaidi.

Ripoti kwa mwaka 2022 inaonesha kuwa deni la umma la kimataifa lilifikia rekodi ya dola trilioni 92 za Kimarekani ambapo nchi zinazoendelea zikionekana kujitwika kiasi kisicho na uwiano.

Fedha nyingi zimeonekana kushikiliwa na wakopeshaji ambao hutoza viwango vya juu vya riba kwa nchi nyingi zinazoendelea. 

“Kwa wastani, nchi za Kiafrika hulipa mara nne zaidi kwa kukopa kuliko Marekani na mara nane zaidi ya nchi tajiri zaidi za Ulaya” amesema Guterres.

Katibu Mkuu wa UN amebainisha kuwa baadhi ya nchi maskini zaidi duniani zinalazimishwa kuchagua kati ya kulipa madeni yao, au kuwahudumia watu wao lakini kwa kuwa madeni hayo yasiyo endelevu yamejilimbikizia katika nchi maskini, hayahukumiwi kuwa hatari ya kimfumo kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa.

Guterres ameieleza hali iliyopo kuwa ni moja ya matokeo ya ukosefu wa usawa uliojengeka katika mfumo wa kifedha wa kimataifa uliopitwa na wakati, ambao unaonesha mienendo ya nguvu ya kikoloni ya enzi ilipoundwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF nchi 36 ziko kwenye kile kinachoitwa "mgogoro wa madeni" au katika hatari kubwa ya dhiki ya madeni. Jumla ya nchi 52, yaani karibu asilimia 40 ya nchi zinazoendelea ziko katika matatizo makubwa ya madeni.../


342/