Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

14 Julai 2023

10:01:41
1379305

Mahakama ya ICC yaanza kuchunguza uhalifu mpya wa kivita nchini Sudan

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Karim Khan, alitangaza jana Alhamisi, kwamba mahakama hiyo imefungua uchunguzi mpya kuhusu "uhalifu wa kivita" huko Darfur, magharibi mwa Sudan.

Tangazo hilo limetolewa baada ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa miili 87 ilizikwa katika kaburi la pamoja katika mji wa El Geneina, katikati mwa jimbo la Darfur Magharibi mwa Sudan, kwa maagizo yaliyotolewa na vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyopigana na jeshi la Sudan.

Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo imelifahamisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba imefungua uchunguzi kuhusu matukio yaliyojiri katika mji wa El Geneina, katikati mwa jimbo la Darfur, ikieleza kuwa ukiukaji wa sheria nchini Sudan unaonyesha kukaririwa historia ya yale yaliyojiri nchini humo miaka iliyopita.

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema."Ninalaani vikali mauaji ya raia na wale wasioweza kupigana vita, na nimeshtushwa na njia za kikatili na za kudhalilisha zilizotumiwa dhidi ya waliouawa, familia zao na jamii." Vilevile ametaka kufanyika uchunguzi wa haraka na wa kina kuhusiana na mauaji hayo.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi ameiambia televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar kwamba, picha na ushahidi vinathibitisha kuhusika kwa wapiganaji wa RSF katika ukiukaji wa sheria huko Darfur, akisisitiza kuwa ofisi hiyo itawasilisha ripoti yake kuhusu ukiukaji huo kwa taasisi hiyo ya kimataifa.

Kwa upande wake, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwamba vikosi vya RSF na wanamgambo washirika waliwanyonga watu wasiopungua 28 katika mji wa Masteri, jimbo la Darfur Magharibi, magharibi mwa Sudan, Mei 28.

Jeshi la Sudan na wapiganaji hasimu wa RSF wanarushiana tuhuma za kuanzisha vita vya ndani vinavyoendelea nchini humo tangu Aprili 15, na kukiuka makubaliano ambayo hayajafanikiwa kukomesha mapigano hayo.

342/