Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

20 Julai 2023

17:02:28
1380887

Kenya, hali si shwari, hofu yatanda katika siku ya pili ya maandano ya Azimio la Umoja

Hali ya taharuki imeendelea kutawala Kenya leo katika siku ya pili ya maandamano yaliyoitishwa na muungano wa Azimio la Umoja–One Kenya linaloongozwa na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga.

Odinga ambaye alishindwa na William Ruto katika uchaguzi uliopita wa Rais amekuwa akisisitiza kuwa, ataendelea kuongoza maandamano dhidi ya serikali kupinga kupanda kwa gharama ya maisha na kwamba, hatalegeza Kamba katika hilo mpaka matakwa yao yatakaposikilizwa.

Vyombo vya habari vya ndani vinaripoti kuwa watu sita waliuawa jana Jumatano katika makabiliano kati ya polisi wa Kenya na waandamanaji.

Makabiliano na ghasia kubwa zilishuhudiwa zaidi katika miji mikubwa ya Nairobi na Mombasa ambako polisi na askari usalama walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi na kuvyatua risasi angani kwa shabaha ya kutawanya waandamanaji.

Shule zilifungwa jana katika miji miwili mikuu nchini humo kwa hofu ya ghasia na maandamano hayo ya siku tatu ambayo leo yameingia siku yake pili leo.

Polisi wamewatia nguvuni waandamanaji wasiopungua 300.Kutokana na machafuko ya sasa nchini Kenya, wahariri wa magazeti ya nchi hiyo wametoa taarifa wakisisitiza haja ya kurejeshwa amani na utulivu nchini huyo. Sehemu moja ya taarifa hiyo imesema: "Kwa sasa, taifa hili limo katika mkondo wa kusambaratika na iwapo hakutakuwa na muafaka na maelewano kuhusu masuala tata, basi nchi itajipata kwenye hali ambayo haitaweza kujinasua." Taarifa wa pamoja na wahariri wa Kenya imesema: Kwa sasa malumbano si muhimu ila hoja kuu ni kuwa, Kenya itaendelea kuteketea kama Rais na Bw Odinga wataendelea kushikilia misimamo mikali. Juhudi za awali za mazungumzo ikiwemo kuundwa kwa kamati ya bunge zimegonga mwamba japo hilo haimaanishi kuwa hakuna nafasi ya kujaribu tena.

342/