Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

20 Julai 2023

17:03:34
1380889

Magaidi 100 wa al-Shabaab waangamizwa katikati ya Somalia

Wanachama wasiopungua 100 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameripotiwa kuuawa katika operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na vikosi vya kigeni katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Wizara ya Habari ya Somalia imesema wanamgambo hao wa al-Shabaab waliuawa katika operesheni kabambe iliyofanyika jana Jumatano katika vijiji vya Gal-Libah na El Quraq vilivyopo katika mpaka wa majimbo ya Galgaduud na Middle Shabelle.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, magaidi hao wakiwemo makamanda wao saba wa ngazi za juu wameuawa katika operesheni ya pamoja ya vikosi vya Somalia kwa ushirikiano na askari vamizi wa Marekani.

Mapema jana pia, Jeshi la Taifa la Somalia lilitangaza habari ya kuangamiza wanachama 30 wa al-Shabaab wakiwemo makamanda wao wawili katika eneo la El Quraq, katikati ya nchi.Taarifa ya maafisa usalama wa Somalia inaeleza kuwa, ngome kadhaa za wanamgambo hao wenye misimamo ya kufurutu ada zimeangamizwa katika operesheni hiyo.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya viongozi wa Somalia kutangaza habari ya kuuawa magaidi 20 wa kundi la wanamgambo wa al-Shabaab katika operesheni ya vikosi vya serikali katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kundi la kigaidi la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya kila liwezalo kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007; na hadi kufikia sasa kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi na kuuwa wanajeshi na raia wengi.  


342/