Main Title

source : Parstoday
Jumatano

26 Julai 2023

15:36:06
1382591

UNESCO yapandekeza marufuku ya simu za mkononi shuleni

Simu za mkononi zinapaswa kupigwa marufuku shuleni ili kusaidia kukomesha usumbufu darasani. Hayo ni kwa mujibu wa mapendekezo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)

Katika taarifa, UNESCO, imesema marufuku hiyo itaboresha masomo na kusaidia kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji mtandaoni.

Utafiti wa UNESCO umebaini kuwa, matumizi mengi ya simu za mkononi yalihusishwa na utendaji duni wa elimu na kwamba muda mrefu unaotumiwa kutizama skrini za simu huvuruga hisia za watoto.

Ripoti hiyo ilmeongeza kuwa, teknolojia ya kidijitali kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na akili bandia (AI) haipaswi kamwe kuchukua nafasi ya "maono yanayomhusu mwanadamu" ya elimu au kuchukua nafasi ya mafundisho ya mwingiliano wa ana kwa ana.

Hali kadhaila UNESCO imesema sio mabadiliko yote yanaleta maendeleo. Ripoti hiyo aidha imetoa wito kwa watunga sera kuzingatia "mwelekeo wa kijamii wa elimu".

Audrey Aloza, mkurugenzi mkuu wa UNESCO amenukuliwa akisema: "Mapinduzi ya kidijitali yana uwezo usiopimika lakini kama maonyo yalivyotolewa kuhusu jinsi yanavyopaswa kudhibitiwa katika jamii tahadhari sawa lazima zizingatiwe kuhusu namna mfumo wa kidijitali unavyotumika katika elimu."

Amesema mapinduzi ya kidijitali lazima yawe kwa ajili ya ustawi wa wanafunzi na walimu, na si kwa madhara yao.

Hali kadhalika mkuu wa UNESCO amesisitiza haja ya kuweka mahitaji ya mwanafunzi katika kipaumbele sambamba na kusaidia walimu katika kazi zao huku akibainisha kuwa matumizi ya mtandaoni sio mbadala wa maingiliano ya wanadamu.

Mwezi uliopita, Ufini ilikuwa nchi ya karibuni barani Ulaya kupiga marufuku simu za mkononi (mobile) darasani katika jaribio la kuzuia kudorara wanafunzi katika masomo hayo. Nchi hiyo imeshuhudia ongezeko la udhaifu katika matokeo ya mitihani na hivyo kutoa udharura wa kupigwa marufu simu za mkononi shuleni.

Muungano mpya wa mrengo wa kulia uliochaguliwa nchini humo uliahidi kuwasilisha sheria mpya ambayo itahakikisha kuna marufukku kamili ya simu za mkononi kwa wanafunzi walio kati ya miaka saba na 15.