Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

29 Julai 2023

20:20:10
1383262

Biden: Kuna uwezekano wa Saudia na Israel kuanzisha rasmi uhusiano wao

Rais wa Marekani, Joe Biden kwa mara nyingine tena amedokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa Saudi Arabia kuanzisha rasmi uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Biden amesema hayo leo Jumamosi akihutubia wafuasi wake katika mkutano wa kampeni katika mji wa Freeport eneo la Maine na kueleza kuwa, mchakato wa kuufanya wa kawaida uhusiano kati ya Saudi Arabia na Israel unaendelea.

Mnamo Julai 9, Biden aliiambia kanali ya CNN kuwa, Saudia na Israel zinaelekea kufikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida; na kwamba mkataba huo utajumuisha ushirikiano wa kiulinzi na kwenye mradi wa nyuklia wa kiraia na Marekani. 

Matamshi ya Biden yamekuja siku mbili baada ya Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani kwenda Jeddah, na kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Saudia, katika ziara ya kuishawishi Riyadh ianzishe uhusiano wa kawaida na Tel Aviv. 

Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal, utawala wa Biden unaendeleza mazungumzo 'magumu' yanayolenga kufanikisha mpango huo wa kuanzishwa uhusiano rasmi kati ya Tel Aviv na Riyadh.

Machi mwaka huu, Saudi Arabia iliiomba Marekani iisaidie katika mpango wake wa kurutubisha madini ya urani ili mkabala wake Riyadh itangaze rasmi kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. 

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, kufikiwa makubaliano kati ya Israel na Saudia ya kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia kunaweza kuzima mwanga wa matumaini ya Wapalestina kuwa na nchi na taifa lao huru. 

342/