Main Title

source : Parstoday
Jumapili

30 Julai 2023

15:05:36
1383596

Niger yazionya nchi za ECOWAS kuhusu kuingilia kijeshi masuala ya ndani ya nchi hiyo

Kiongozi mpya wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahmane Tchiani ameionya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) na washirika wake dhidi ya kuingilia kijeshi masuala ya nani ya Niger.

ECOWAS inafanya mkutano wa dharura kuhusu hali nchini Niger, ambapo jeshi lilimuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum. Mkutano huo unafanyika leo katika mji mkuu wa nchi jirani ya Nigeria, Abuja.

Tchiani ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba:"Tunaionya ECOWAS na washirika wake dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi katika jiji la Niamey. Wakifanya hivyo tutalazimika kujilinda hadi mwisho wa nguvu zetu,"

Siku ya Ijumaa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walitoa wito wa kuachiliwa mara moja na bila masharti rais aliyechaguliwa kidemokrasia wa Niger Mohammed Bazoum na kusisitiza haja ya kumlinda yeye, familia yake na watu wa serikali yake.

Jumatano, 26 Julai, kundi la maafisa wa kijeshi wa Niger kupitia televisheni walitangaza mapinduzi, baada ya walinzi wa rais kumweka kizuizini ndani ya ofisi yake katika mji mkuu wa Niger, Niamey. Awali jaribio hilo la mapinduzi halikuungwa mkono na jeshi zima, lakini mkuu wa jeshi akatangaza kwamba anaunga mkono hatua hiyo.

Katika taarifa yao, wajumbe wa Baraza la Usalama wameeleza wasiwasi wao kuhusu athari mbaya za mabadiliko ya kikatiba ya serikali katika eneo hilo, ongezeko la vitendo vya kigaidi na hali mbaya ya kijamii na kiuchumi. Pia wamesisitiza masikitiko yao kuhusu matukio ya Niger, ambayo yanadhoofisha juhudi za kuunganisha taasisi za utawala na amani katika nchi hiyo.  

342/