Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

31 Julai 2023

17:04:49
1383947

Kwa nini Marekani ina hasira kuhusu ushirikiano kati ya China na Russia?

Serikali ya China imetetea uhusiano wake na Russia, na kusema uhusiano huo ni katika fremu ya ushirikiano wa kawaida wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, Marekani na washirika wake wanajaribu kuweka mashinikizo zaidi kwa nchi hiyo kupitia madai ya kisiasa na vyombo vya habari kuhusu msaada wa kijeshi wa China kwa Russia. China imekuwa ikiionya mara kwa mara Marekani na kuitaka isiingilie mambo yake ya ndani na uhusiano wake wa kigeni. Hata hivyo Marekani na washirika wake, ambao wanakabiliwa na matatizo makubwa katika vita vya Ukraine, ikiwa ni pamoja na kurefuka kwa vita hivyo na shinikizo la bajeti linalosababishwa na misaada ya hali na mali ya nchi za Magharibi kwa serikali ya Kiev, zinajaribu kuitambulisha China na nchi nyingine kuwa ndiyo sababu ya mafanikio ya Russia katika vita vya Ukraine, na kwa namna fulani, kuhalalisha kushindwa kwao katika vita hivyo. Kwa msingi huo, katika mkutano wa Mei wa viongozi wa G7 uliofanyika nchini Japani, sambamba na kuweka vikwazo zaidi dhidi ya Russia, viongozi wa kundi hilo walitoa misaada zaidi ya kijeshi kwa serikali ya Ukraine kwa ajili ya kupambana na Russia.

Hei Sing Tso, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema: “Mbali na kujaribu kuidhoofisha Russia katika vita vya Ukraine, Marekani pia inafuata sera ya kuidhoofisha China. Kwa kutoa shutuma dhidi ya China, Marekani inatekeleza sera mbili zinazoilenga Russia na China na nchi nyingine ambazo zina uhusiano na Russia. Wakati huo huo, China na nchi nyingine huru zinatetea uhusiano wao na Russia kulingana na kaida na kanuni za kimataifa."

Vyombo vya habari vya Marekani hivi karibuni vilidai kuwa data za Idara ya Forodha ya Russia zinaonyesha kwamba, wakandarasi wa kijeshi wa serikali ya China wametuma bidhaa za matumizi ya kijeshi kwa Russia, ikiwa ni pamoja na vifaa vya meli za kivita, vipuri vya ndege za kijeshi, droni na bidhaa zingine. Hii ni licha ya kuwa, kwa mujibu wa Mao Ning, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, nchi hiyo ina ushirikiano wa kawaida wa kibiashara na kiuchumi na nchi zote za dunia, ikiwa ni pamoja na Russia. Marekani ambayo ndiyo sababu kuu ya kuanza vita vya Ukraine, inajiona yenyewe na washirika wake, ajizi na dhaifu dhidi ya Russia, hivyo inazituhumu nchi mbalimbali kuwa zinaisaidia kuimarisha nguvu zake za kijeshi. Marekani hadi sasa imetoa mabilioni ya dola kama msaada kwa Ukraine, na hivi karibuni kabisa imetuma mabomu ya vishada kwa nchi hiyo.

Mtaalamu wa masuala ya kimataifa, Daniel Kowalik, anasema: Marekani na washirika wake hawakufikiria kabisa kwamba vita vya Ukraine vingechukua muda mrefu. Hali hii ambayo inautwisha uchumi wa nchi za Ulaya mzigo mkubwa wa bajeti, polepole inasababisha maandamano ya wananchi katika nchi hizo, jambo ambalo linaiweka Marekani na washirika wake katika matatizo zaidi ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine.

Vyovyote iwavyo, ili kusaidia kutatua mzozo wa Ukraine, China ilipendekeza mpango wa suluhu wenye vifungu 12 kwa ajili ya kumaliza vita, jambo ambalo lilipingwa na Marekani. Kabla ya kuanza vita vya Ukraine mnamo Februari 24, 2022, Rais wa China, Xi Jinping na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin walitangaza urafiki usio na kikomo baina ya nchi hizo mbili. Kwa hivyo, licha ya kutangaza kutoegemea upande wowote katika vita vya Ukraine, Beijing imezuia juhudi za nchi za Magharibi za kuilaani Russia katika Umoja wa Mataifa na imeunga mkono sababu za Moscow katika vita vya Ukraine.Katika mpango wake wa amani, Beijing imesisitiza kuanza kwa mazungumzo ya amani kati ya Moscow na Kiev, kusitisha mapigano, kukomeshwa vikwazo vya Magharibi dhidi ya Russia, kuchukuliwa hatua za kuhakikisha usalama wa vituo vya nyuklia na hatua za kudhamini usafirishaji wa nafaka nje ya nchi ya Ukraine. Marekani na washirika wake walikataa mpango huo kwa kisingizio kwamba unaipendelea Russia, jambo ambalo limesababisha kuendelea na kushadidi vita vya Ukraine. Wakati huo huo, mashinikizo ya kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani kwa Uchina na washirika wengine wa kibiashara wa Russia hayajaweza kudhoofisha nafasi ya nchi hiyo. Kwa msingi huo, Marekani bado inajaribu kuchochea maoni ya umma dhidi ya China na washirika wengine wa Russia kupitia mashambulizi ya vyombo vya habari.