Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

4 Agosti 2023

17:18:36
1384772

Pendekezo la Russia: Washington, London na Paris zinapaswa kuilipa fidia Afrika

Mkuu wa Duma ya Russia amesema kuwa, Marekani, Uingereza na Ufaransa zinapaswa kulipa fidia kwa bara la Afrika kwa uharibifu ambao zimeufanya barani humo.

Vyacheslav Volodin, mkuu wa Bunge la Duma la Russia, ameutaka  Umoja wa Mataifa kuchunguza suala la Marekani, Uingereza na Ufaransa kulipa fidia kwa watu wa bara la Afrika kutokana na hasara na uharibifu uliosababishwa na nchi hizo kwa watu wa bara hilo.

Volodin amesisitiza kuwa: Afrika ina haki ya kujitegemea katika kufaidika na uutajiri na rasilimali zake na kudai fidia kwa uharibifu uliosababishwa na wakoloni.

Kabla ya hapo Russia ilikuwa imekosoa matamshi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye alilitaja pendekezo la Moscow la kutoa nafaka bure kwa baadhi ya nchj za Afrika kuwa ni "kitu kidogo".

Itakumbukwa kuwa, tarehe 26 Julai, Kikosi cha Ulinzi wa Rais wa Niger kilimuondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Mohamed Bazoum, ambaye ana uhusiano wa karibu sana na Ufaransa, na kutwaa madaraka ya nchi.

Ingawa Niger ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, lakini ina akiba kubwa zaidi ya uranium, na kwa sasa uranium inayotolewa huko Niger inazalisha 35% ya nishati ya nyuklia na 75% ya umeme wa Ufaransa, wakati asilimia kubwa ya Waniger wenyewe hawana umeme. 

342/