Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

5 Agosti 2023

19:07:12
1385019

CIA inahariri Wikipedia katika 'vita vya habari'

Serikali ya Marekani na mashirika yake ya kiusalama likiwemo shirika lake kuu la kijasusi, CIA hutumia mtandao wa Wikipedia kama mojawapo ya zana zake kuendesha "vita vya habari." Hayo yamefichuliwa na mwanzilishi mwenza wa tovuti hiyo, Larry Sanger.

Sanger amemwambia mwandishi wa habari mpelelezi wa Marekani Glenn Greenwald kwamba mashirika ya kijasusi yamekuwa yakidhibiti ensaiklopidia ya mtandaoni ya Wikipedia kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Sanger amesema Wikipedia imekuwa chombo cha kudhibiti fikra mikononi mwa mashirika ya kiusalama ya Marekani, hasa  CIA na  FBI, na pia mashirika mengine ya kijasusi ya nchi hiyo.

Amesema, "Tuna ushahidi kwamba, kuanzia 2008,  kompyuta za CIA na FBI zilitumiwa kuhariri Wikipedia," na ameendelea kwa kuhoji hivi, "Je, unafikiri kwamba waliacha kufanya hivyo wakati huo?"

Mwanafunzi wa programu za kompyuta anayeitwa Virgil Griffith alichapisha kwa mara ya kwanza shughuli ya CIA na FBI ndani ya Wikipedia mnamo 2007. Griffith alianzisha programu ambayo inaweza kufuatilia eneo la kompyuta zinazotumiwa kuhariri makala za Wikipedia.

Aligundua kuwa CIA, FBI, na mashirika mengine kadhaa ya serikali ya Marekani yalikuwa yakichambua ensaiklopidia hii ya mtandaoni na kuondoa maelezo ambayo yalikuwa dhidi ya Marekani.

Imedokezwa kuwa, CIA ilitumia kompyuta zake kuondoa idadi ya watu waliopoteza maisha katika Vita vya Iraq, huku FBI ikiondoa picha za angani na satelaiti za jela ya kijeshi ya Marekani huko Guantanamo Bay nchini Cuba.

CIA ilitumia kompyuta zake kuhariri mamia ya makala, ikiwa ni pamoja na maandishi kuhusu rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, mpango wa nyuklia wa China, na jeshi la wanamaji la Argentina.

Kwa kuongezea, mkuu wa zamani wa CIA William Colby hata alihariri ingizo lake mwenyewe ili kuongeza orodha yake ya mafanikio.

Sanger amemwambia Greenwald kwamba," Mashirika ya kijasusi hulipa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi kusukuma ajenda zao.

Aidha amesema sehemu kubwa ya vita vya kijasusi na habari vinaendeshwa mtandaoni kwenye tovuti kama Wikipedia.

342/