Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

5 Agosti 2023

19:07:48
1385020

Sisitizo la Rais wa Brazil la kupigwa teke sarafu ya dola katika biashara za kimataifa

Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil ametaka kupigwa teke na kuwekwa pembeni matumizi ya sarafu ya dola katika biashara za kimataifa na kutafutwa sarafu nyingine za kuziba nafasi ya sarafu hiyo ya Marekani.

Rais wa Brazil alitoa mwito huo Jumatano na kusisitiza kwamba nchi wanachama wa kundi la BRICS ambazo ni Afrika Kusini, Russia, India, China na Brazil zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha jukumu hilo muhimu. 

Rais Lula da Silva alisema: Kila mmoja anatambua kuwa mimi ni muungaji mkono wa nchi kutumia sarafu zao kufanyia miamala ya kibiashara baina ya mataifa mbalimbali duniani. Wakati sisi kwa mfano tunapofanya biashara na Argentina na China, kwa nini tulazimike kutumia sarafu ya dola wakati tunaweza kiurahisi tu kutumia fedha zetu wenyewe katika miamala hiyo?  Kwa nini nchi ambazo zina takriban nusu ya watu duniani zinashindwa kufikia uamuzi wa maana katika jambo hilo?Kabla ya hapo pia, Rais Vladimir Vladimirovich Putin wa Russia wakati alipozungumza na Gavana wa Benki Mpya ya Maendeleo ya kundi la BRICS, Bi Dilma Vana Rousseff alisisitiza kuwa, benki hiyo ya BRICS ina jukumu la kuweka mfumo wa kutumiwa sarafu nyingine katika miamala ya kimataifa. Alisema, kuanzisha taasisi za fedha za kushika nafasi ya taasisi zilizopo hivi sasa katika wakati huu ambapo Washington inatumia dola ya Marekani kama silaha, ni jambo zito lakini ni la dharura.

Kampeni ya kuipiga vita sarafu ya dola ya Marekani imeshika kasi hivi sasa na iliingia kasi zaidi mwaka 2007. Hivi sasa nchi nyingi duniani zimekuja na wazo la kuachana na matumizi ya sarafu ya dola kwenye miamala yao ya kibiashara. Katika kipindi cha miaka ya 2007 na 2008 kulizuka mgogoro mkubwa wa kiuchumi duniani. Wakati huo na kwa mara ya kwanza, nchi za Russia, China na za Amerika ya Latini zilianza rasmi kufanyia majaribio matumizi ya sarafu zao wenyewe katika miamala yao ya kibiashara.

Tatizo jengine ambalo ni kubwa zaidi ni kwamba kwa vile sehemu kubwa ya miamala ya kibiashara duniani inafanyika kwa sarafu ya dola, Marekani imeibadilisha sarafu hiyo kuwa silaha dhidi ya mataifa ambayo hayapendi kuburuzwa na dola hilo la kiistikbari. Inatumia sarafu ya dola kujaribu kutoa pigo kwa nchi wapinzani na maadui zake bila ya kujali madhara ya vita vyake hivyo vya kiuchumi. Kwa kweli Marekani imekuwa ikiitumia sarafu ya dola kama silaha yake kuu ya kuyashinikiza mataifa mengine katika miamala ya kimataifa ya fedha. Ijapokuwa hadi hivi sasa dola inahesabiwa kuwa sarafu kubwa zaidi katika akiba ya fedha ya benki za dunia, lakini kitendo cha Marekani cha kutumia sarafu hiyo kama silaha kimepelekea kuongezeka kasi ya nchi za duniani ya kuacha kutumia sarafu hiyo katika miamala yao ya kibiashara. Miongoni mwa nchi hizo ni wanachama wa Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia ambazo zimeamua kuipiga teke sarafu ya dola katika miamala yao yote ya kibiashara na kifedha. Hatua hiyo imepata nguvu hasa baada ya Marekani kuanzisha kuiwekea vikwazo Russia katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita wa tangu kuanza vita vya Ukraine. Zaidi ya hayo nchi kama China, India na Uturuki zimeonesha wazi kuwa haziko tayari kushiriki katika vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia na ndio maana nazo zimeingia kwenye mkondo wa kutumia sarafu zao za ndani katika miamala yao na kuachana na sarafu ya dola. Bi Elvira Sakhipzadovna Nabiullina, Gavana wa Benki Kuu ya Russia kwa upande wake amesema, moja ya sababu za kuingia kasi vita dhidi ya sarafu ya dola katika uchumi wa nchi yake ni vikwazo vya Marekani. Amesema: 'Ninahisi hali ya mambo ya kimataifa inabadilika. Pole pole tunaona dunia inaelekea kwenye mfumo wa kifedha wa sarafu kadhaa.'  Kuendelea Marekani kutumia vibaya sarafu ya dola kama silaha ya vita vya kiuchumi dhidi ya mataifa mengine kunazidi kuongeza azma ya mataifa yanayostawi haraka kiuchumi duniani kutafuta sarafu nyingine za kufanyia biashara zao na hilo kwa hakika ni pigo kubwa kwa Marekani. Mwaka 2015 wakuu wa kundi la BRICS yaani wa nchi za Afrika Kusini, Russia, Brazil, India na China walitangaza kuwa wameamua kutumia fedha zao wenyewe katika mabadilishano ya kibiashara na kuchukua hatua za kimsingi za kupunguza kutegemea sarafu ya dola. Baada ya nchi wanachama wa Eurasia kutangaza kuwa zimeanza kutekeleza rasmi sera ya kutumia sarafu za taifa katika mabadilishajo yao ya kibiashara ikiwa ni hatua muhihmu nyingine ya kuipiga teke sarafu ya dola ya Marekani, mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu wa 2023 pia, nchi nyingine mbili muhimu za kundi la G20 yaani Brazil na China ambazo zina uchumi mkubwa duniani na ni wanachama wa BRICS ziliamua kuanza kutekeleza rasmi jambo hilo. Tarehe 29 mwezi huo wa Machi, nchi hizo mbili zilitangaza kuwa zimeipiga 'buti' sarafu ya dola ya Marekani na sasa zitakuwa zinatumia sarafu zao wenyewe katika mabadilishano yao ya kibiashara.

342/