Main Title

source : Parstoday
Jumanne

8 Agosti 2023

18:21:04
1385683

Rais wa Venezuela awakosoa watawala wa Ulaya kwa kukaa kimya kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amewakosoa vikali watawala wa nchi za Ulaya kutokana na ukimya wao kuhusu vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Uswidi na Denmark.

Katika mahojiano na mtandao wa habari wa televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon siku ya Jumatatu, Maduro amesema: "Ninalaani vitendo hivi vya kibaguzi vya chuki dhidi ya mataifa ya Kiislamu."

Kiongozi huyo wa Venezuela amesema: "Kimya cha viongozi wa Ulaya juu ya kuchomwa kwa nakala za Qur'ani kinashangaza, na kimya hicho ni sawa na kushiriki kwao katika uhalifu huo."

Maduro amesema haiwezekani kufumbia macho chokochoko hizo zinazodhalilisha Uislamu na wafuasi wake.

Rais wa Venezuela ameendelea kwa kuhoji hivi, "Je, Wakristo wa Ulaya wangesema nini ikiwa Biblia ingechomwa moto mbele yao?"

Rais wa Venezuela amesema ni "kawaida kabisa" kwamba jumuiya ya Kiislamu duniani imeonyesha "mtazamo wa hasira" kwa kudhalilishwa kitabu hicho kitakatifu.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, Qur'ani Tukufu imekuwa ikikabiliwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima  mara kadhaa na watu wenye misimamo mikali nchini Uswidi na Denmark, huku serikali za nchi hizo zikiidhinisha na kuhalalisha vitendo hivyo viovu kuwa ni "uhuru wa kujieleza."

Vitendo hivyo dhidi ya Qur'ani Tukufu vimechochea hasira ya jamii nzima ya Waislamu duniani kote.

342/