Main Title

source : Parstoday
Jumatano

9 Agosti 2023

19:02:59
1385904

Kukosoa Maduro kimya cha viongozi wa Ulaya kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amekosoa vikali kuendelea kukaa kimya viongozi wa Ulaya kuhusiana na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Katika radiamali yake kwa vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu Rais Maduro amesema, anasikitishwa mno na kimya kikubwa cha viongozi wa Ulaya mbele ya matukio ya kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na mtandao wa habari wa televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon siku ya Jumatatu, Maduro amesema: "Ninalaani vitendo hivi vya kibaguzi na vya chuki dhidi ya mataifa ya Kiislamu."

Kiongozi huyo wa Venezuela amesema: "Kimya cha viongozi wa Ulaya juu ya kuchomwa kwa nakala za Qur'ani kinashangaza, na kimya hicho ni sawa na kushiriki kwao katika uhalifu huo."

Rais wa Venezuela amesema: Ninawauliza Wakristo wa ulimwengu, je, tutajisikiaje ikiwa watu watachukua hatua ya kuchoma moto kitabu kitakafu cha Wakristo huko Sweden au Denmark au nchi nyinginezo?

Rais wa Venezuela ameashiria kadhia hiyo na kubainisha kwamba, nikiwa Mkristo, najiuliza sisi Wakristo tungehisije mtu akijaribu kuchoma Biblia? Bila shaka tutakasirika sana na itakuwa tusi na uvunjiaji heshima mkubwa mtu akichoma maandiko ya kitabu hiki. Ndani ya moyo wangu, ninaelewa na kudiriki hasira ya Waislamu duniani kote wanapoona Qur'ani Tukufu ikichomwa moto.Msimamo wa wazi wa Rais wa Venezuela kuhusiana na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya hususan Sweden na Denmark unaonyesha kuwa, licha ya madai ya viongozi wa Ulaya wakiwemo wa Sweden na Denmark kuhusu kutozuia kuchomwa moto Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza, ni jambo ambalo halikubaliki kwa vyovyote vile miongoni mwa wakuu wa nchi zinazopinga ubeberu na thamani za Magharibi, kama vile Venezuela.

Licha ya radiamali kubwa za Waislamu na mataifa ya Kiislamu kuhusu suala la Qur'ani kuchomwa moto katika nchi mbili za kaskazini mwa Ulaya, yaani Sweden na Denmark, na upinzani wa wazi wa Umoja wa Mataifa dhidi ya hatua hiyo ya udhalilishaji, na hata ahadi za mamlaka za nchi hizi mbili za kuzuia vitendo kama hivyo, lakini wenye chuki dhidi ya Uislamu wangali wanaendeleza vitendo vyao vya kishenzi vya kukivunjia heshima kitabu hiki kitakatifu cha Waislamu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Rais Maduro sanjari na kukosoa chuki dhidi ya Waislamu amesisitiza kuwa,  makundi ya mrengo wa kulia yenye kufurutu ada na ya kibaguzi katika mataifa ya Magharibi ambayo yanachukua hatua za kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu yanapaswa kulaaniwa.

Licha ya radiamali kali za Waislamu, mataifa ya Kiislamu na hata Umoja wa Mataifa dhidi ya mamluki wa Uzayuni kama Momika Salwan ambaye mfungamano wake na Tel Aviv ni jambo lisilo na shaka, lakini mataifa ya Magharibi yangali yanatoa idhini kwa watu wenye chuki na Uislamu kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu hususan kuchomwa moto Qur'ani Tukufu.Hadi sasa Momika amejitokeza hadharani na kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mara tatu. Licha ya hayo, lakini bado mataifa ya Magharibi yameendelea kutoa kibali kwa makundi yenye chuki na Waislamu cha kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu hususan kuchomwa moto Qur'ani Tukufu kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza. Himaya na uungaji mkono wa Wamagharibi kwa kitendo cha kuvunjiwa heshima na cha kuchomwa moto Qur'ani unafanyika katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa unapinga kitendo hicho cha aibu. Farhan Haq, Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema: Miguel Moratinos, Mkuu wa Asasi ya Staarabu ya Umoja wa Mataifa amelaani vikali kuchomwa moto Qur'ani Tukufu mbele ya msikiti mmoja katikati ya mji wa Stockholm, Sweden. Inaonekana kuwa, Wamagharibi wanapuuza kwa makusudi tofauti baina ya uhuru wa kusema na kutusi matukufu ya dini. Tukitupia jicho vigezo vya kindumakuwili vya madola Magharibi zikiwemo Sweden na Denmark kuhusiana na uhuru wa kutoa maoni tunaona kuwa, jambo hili hubeba maana pale tu linapohoji na kuvunjia heshima jambo ambalo ndio mtazamo wa Magharibi kama vile chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu. Lakini mambo ni kinyume kabisa kuhusiana na masuala mengine kama ngano ya Holocaust. Mfano mwingine wa wazi ni vita vya Ukraine na Russia ambapo wanaotoa maoni na mitazamo kuhusu vita hivyo ambayo ni kinyume na matazmo wa madola ya Magharibi hukabiliwa na mashinikizo ya kila upande na wakati mwingine kukabiliwa na mashtaka kama ilivyo katika suala la Holocaust. Hapana shaka kuwa, ukosoaji mkali wa Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kwa kimya cha viongozi wa Ulaya kuhusiana na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa mara nyingine tena umeweka wazi utambulisho wa kindumakuwili wa vigezo vya madola ya Magharibi kuhusiana na uhuru wa kusema au wa kutoa maoni.

342/