Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Agosti 2023

16:58:59
1386365

Kujinyonga ndiyo sababu ya pili kuu ya vifo nchini Marekani

Takwimu za karibuni kabisa zilizotolewa na serikali ya Marekani zinaonesha kuwa, kesi za watu wanaojinyonga na kujikatishia maisha katika nchi hiyo ya Magharibi inayojilabu kuwa na maisha bora duniani, zilivunja rekodi mwaka 2022 kiasi kwamba kujiua kumeshika nafasi ya pili ya sababu za vifo nchini humo.

Ongezeko la vitendo vya watu kujinyonga na kujikatishia maisha ndiyo daghadagha na wasiwasi mkubwa wa kitaifa nchini Marekani kiasi kwamba takwimu za madaktari nchini humo zinaonesha kuwa, kujinyonga ni sababu ya pili kuu ya vifo kwa watu wa umri wa kuanzia miaka 5 hadi 24 nchini humo. Tukumbuke kuwa, Marekani ni nchi ambayo inajigamba kuwa wananchi wake wana matumaini makubwa ya kuishi maisha ya raha na anasa.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu waziri wa afya wa Marekani, Xavier Becerra akitoa takwimu za kutisha zinazoonesha kuwa, kati ya kila Wamarekani 10, 9 kati yao wanaamini kwamba Marekani imetumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa maradhi ya kiakili na kisaikolojia. Takwimu mpya za vitendo vya kujikatishia maisha nchini Mraekani ni ushahidi wa wazi wa uhakika huo.Kwa upande wake Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani kimetangaza kuwa, zaidi ya nusu ya kesi 50,000 za kujiua zilifanyika kwa kutumia silaha moto nchini Marekani mwaka 2022. Takwimu za kituo hicho zinaonesha kuwa, mwaka 2021 kulirekodiwa kesi 48,183 za watu kujiua huko Marekani, takwimu ambazo bila ya shaka yoyote haziakisi kiwango halisi cha kesi hizo na ni wazi kwamba idadi ya watu wanaojiua nchini Marekani ni zaidi ya hiyo inayotolewa na taasisi rasmi za serikali. Vifo hivyo havijumuishi mauaji ya kiholela ya watu wasio na hatia yanayofanyika kila siku nchini Marekani kwa kutumia silaha moto na ambayo yanafanywa na watu waliochoshwa na maisha. Kwa miaka mingi sasa sehemu kubwa ya Wamarekani wanalalamikia uhuru wa kumiliki na kubeba silaha kiholela nchini humo na wamekuwa wakitilia mkazo mno kurekebishwa sehria hiyo. Lakini makundi yenye nguvu na yanayofaidika mno na uuzaji silaha hadi sasa yamekuwa kikwazo kikubwa cha kupasishwa sheria ya kudhibiti matumizi na ubebaji silaha kiholela huko Marekani.

342/