Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Agosti 2023

16:59:33
1386366

Polisi wa Ecuador: Wauaji wa mgombea urais, Villavicencio, wametokea Colombia

Polisi wa Ecuador wamesema kwamba wahusika wa mauaji ya mgombea urais, Fernando Villavicencio walitokea Colombia, huku serikali ikiahidi kufuatilia "wapangaji" wa mauaji hayo ambayo yalitikisa nchi hiyo Jumatano wiki hii.

Fernando Villavicencio alipigwa risasi na kuuawa katika mkutano wa kisiasa kwenye mji mkuu wa Ecuador, Quito siku ya Jumatano, tukio lililosababisha mshtuko katika nchi hiyo, ambayo inatazamiwa kufanya uchaguzi wa rais tarehe 20 mwezi huu wa Agosti. Mwanasiasa huyo alipigwa risasi tatu kichwani.

Mgombea huyo alikuwa mkosoaji mkubwa wa ufisadi na vikundi vya ulanguzi wa dawa za kulevya ambavyo vimepata ushawishi mkubwa nchini Ecuador katika miaka ya hivi karibuni.

Polisi wa Ecuador wamewakamata washukiwa sita, ambao wote ni raia wa Colombia. Mshukiwa wa saba aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumatano.

Saa chache baada ya mauaji hayo, Rais Guillermo Lasso wa Ecuador alilaumu mitandao ya uhalifu kuwa ndiyo iliyohusika na vurugu hizo.Kipindi fulani, Ecuador ilitambuliwa kuwa chanzo cha utulivu wa kiasi katika eneo lenye historia ndefu ya vurugu na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe. Hata hivyo katika miaka kadhaa iliyopita, nchi hiyo imeshuhudia ongezeko la uhalifu.

342/