Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

11 Agosti 2023

17:03:19
1386373

IGP wa Tanzania atoa onyo kali kwa wanaochochea maandamano kwa lengo la kuipindua Serikali

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Camillus Wambura amesema, kuna kundi la watu ambao wamepanga kuandaa maandamano nchi nzima ili kuiangusha Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya awamu ya sita kabla ya mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam IGP Wambura amesisitiza kuwa watu hao ambao wamefanya kosa la uhaini kwa kauli yao hiyo, wanahusisha maandamano hayo na kuwashawishi Watanzania kuwaunga mkono na hoja zinazoendelea kuhusu mkataba wa uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam.

Amesema, aliamini kwa vile baadhi ya watu hao walienda mahakamani, wangehishimu mahakama, lakini badala yake wametoka na kuanza kutafuta ushawishi na kuchochea kuwataka Watanzania waingie kwenye maandamano ya nchi nzima.

"Lakini mmoja amekwenda mbali zaidi na kusema watahakikisha wanaiangusha serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya mwaka 2025. Huu ni uhaini", amesisitiza mkuu huyo wa jeshi la Polisi.IGP Wambura amewaonya watu hao kwamba wakome na wasitishe matamshi yao hayo ya kichochezi, lakini pili amesema, watachukuliwa hatua za kisheria kutokana na uchochezi wanaoufanya na uhaini wanaoupanga, kwani vyote ni makosa ya jinai. Kauli hiyo ya IGP Wambura imekuja siku moja baada ya Wakili Boniface Mwabukusi kutangaza kuwa wataandaa maandamano yasiyo na ukomo nchi nzima iwapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halitafanyia marekebisho vifungu vya mkataba wa bandari ndani ya siku 14. Mwabukusi ametoa kauli hiyo baada ya jana Agosti 10 Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya kutoa hukumu ya kutupilia mbali hoja sita zilizowasilishwa na wakili huyo aliyewakilisha wananchi wanne waliofungua kesi ya kikatiba kupinga baadhi ya vifungu vya mkataba huo.../

342/