Main Title

source : Parstoday
Jumapili

13 Agosti 2023

17:38:37
1386796

China yaapa kuchukua 'hatua za utumiaji nguvu' sambamba na makamu wa rais wa Taiwan kuwasili Marekani

China imeahidi kuchukua "hatua madhubuti na za nguvu" kulinda mamlaka yake baada ya Makamu wa Rais wa Taiwan William Lai kuwasili Marekani kwa ziara fupi.

Kauli hiyo ambayo imetolewa kupitia taarifa mapema leo, imekuja saa chache baada ya Lai kuwasili New York kwa kile kilichodaiwa rasmi kama kituo cha kisimamo cha muda akiwa njiani kuelekea Paraguay.Katika taarifa hiyo iliyotolewa muda mfupi baada ya Lai kutua New York kwa ndege kutoka Taipei, wizara ya mambo ya nje ya China ilisema, inapinga aina yoyote ya ziara ya "wanaotaka kujitenga kwa kupigania uhuru wa Taiwan" kuelekea Marekani.

Taarifa hiyo ya wizara ya mambo ya nje ya China imeendelea kueleza kwamba, Taiwan ni "kiini cha maslahi ya msingi ya China" na ukweli umeonyesha tena na tena kwamba sababu ya kuongezeka mvutano katika Langobahari la Taiwan ni Taiwan kujaribu "kuitegemea Marekani kwa ajili ya kupigania kujitawala".Katika taarifa yake hiyo, Beijing imesisitiza kuwa, inafuatilia kwa karibu kila kinachoendelea na itachukua hatua kali na madhubuti kutetea mamlaka yake ya kujitawala na umoja wa ardhi yake yote. William Lai, anayepewa nafasi kubwa ya kuwa rais ajaye wa Taiwan katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Januari, yuko njiani kuelekea Paraguay kuhudhuria kuapishwa Rais mteule Santiago Pena na amepangiwa kusimama mara ya pili katika jiji la San Francisco nchini Marekani wakati akirejea Taipei. Serikali ya China ambayo inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake imeshalaani mara kadhaa ziara hiyo ya Lai. Makamu huyo wa rais wa Taiwan amekuwa mzungumzaji mkali zaidi wa kupigania kujitawala kisiwa hicho kuliko hata Rais wake Tsai Ing-wen, ambaye tayari ana mvutano na Beijing kwa kuukataa mtazamo kwamba Taiwan ni sehemu ya China.../

342/