Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

14 Agosti 2023

20:32:42
1387067

Sababu za kuongezeka jinai za genge la kigaidi la Daesh nchini Syria

Genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kwa mara nyingine tena limeongeza operesheni zake za kigaidi nchini Syria.

Hivi karibuni magaidi wa ISIS wamefanya mashambulizi nchini Syria hususan katika maeneo ya mpakani mwa nchi hiyo. Magaidi wa Daesh walisambaratishwa kutimuliwa nchini Syria mwaka 2019 baada ya kukombolewa maeneo ya nchi hiyo ya Kiarabu yaliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na magaidi hao kwa msaada wa madola ya kiistikbari. 

Jumanne iliyopita, magaidi wa Daesh walifanya shambulio katika eneo la Ma'dan 'Atiq, mashariki mwa mkoa wa Raqqah nchini Syria dhidi ya basi lililokuwa limebeba makuruta wa jeshi la Syria na kuua askari 10 katika shambulio hilo la kuvizia. Alkhamisi iliyopita pia, genge hilo la ukufurishaji lilifanya shambulio jingine dhidi ya basi lililokuwa na makuruta wa jeshi la Syria katika mkoa wa Deir ez-Zur wa mashariki mwa nchi hiyo na kuua askari 20 na kujeruhi wengine 10. Hilo lilikuwa shambulio lililosababisha vifo vingi zaidi vya askari wa Syria  tangu mwanzoni mwa mwezi huu Agosti. Tarehe 27 mwezi uliopita wa Julai pia, magaidi wa ISIS waliripua pikipiki iliyotegwa mabomu karibu na gari moja moja kwenye eneo ilipo Haram ya Bibi Zainab SA kusini mwa Damascus, mji mkuu wa Syria na kuua shahidi Waislamu 6 na kujeruhi wengine 21. Swali muhimu linalojitokeza hapa ni kwamba ni sababu gani zilizopelekea magaidi wa ISIS wazidishe mashambulizi yao ya kigaidi nchini Syria hivi sasa? 

Inavyoonekana sababu ya kwanza kabisa ni kwamba magaidi hao wanataka kuonesha kuwa bado wako nchini Syria. Hasa kwa kuzingatia kuwa, viongozi wanne wakuu wa genge hilo ambao waliliongoza mtawalia, wameshaangamizwa mmoja baada ya mwingine tangu genge hilo liliposhindwa kijeshi huko Syria na Iraq. Hivi karibuni pia, genge hilo lilithibitisha kuangamizwa kiongozi wake mwingine aliyejulikana kwa jina bandia la Abul Husain al Husaini al Qurashi katika mapigano yaliyotokea Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria. Genge hilo limemtangaza Abu Hafs al Hashimi al Qurashi kuwa kiongozi wake mpya. 

Hivyo jinai zinazofanywa hivi sasa na genge la ukufurishaji la ISIS huenda zinatokana na kujaribu kulipiza kisasi cha kuangamizwa mfululizo viongozi wakuu wa genge hilo. Wachambuzi wa mambo wanatabiri kuendelea pia jinai hizo za genge la kigaidi la Daesh katika siku zijazo kwa shabaha na lengo hilo hilo. Rami Abdul Rahman, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Haki za Binadamu la Syria anasema: Genge la Daesh limeongeza mashambulizi yake hivi sasa nchini Syria ili kuonesha kuwa bado lipo licha ya kupoteza mtawalia, viongozi wake wakuu.Sababu ya pili ya kuongezeka jinai za genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh huko Syria linahusiana na siasa za Marekani. Ongezeko la mashambulio ya magaidi wa ISIS kwenye maeneo tofauti ya Syria linashuhudiwa katika hali ambayo hadi hivi sasa ripoti nyingi zilizotolewa na duru za kieneo zinaonesha kwamba, jeshi la Marekani linawahamishia Syria magaidi wa Daesh waliofungwa jela katika maeneo mengine. Magaidi hao wanapelekwa kwenye kambi za kijeshi za Marekani na kupewa mafunzo maalumu ya kufanya vitendo vya kigaidi pamoja na silaha na zana nyinginezo za kivita. Marekani haitaki kuona utulivu unapatikana huko Syria kwani itakosa kisingizio cha kuendelea kubakia wanajeshi wake vamizi nchini humo. Wizi wa mafuta na utajiri mwingine wa Syria ni sababu nyingine inayoifanya Marekani iwatumie vibaraka wake kama magaidi wa ISIS kuvuruga usalama wa nchi hiyo ya Kiarabu ili izidi kuiba utajiri wake. Kiujumla ni kwamba wananchi wa Syria wanaishinikiza Marekani iondoke nchini mwao kwa sababu kwanza imeingia kivamizi bila ya idhini ya serikali halali ya Syria wala Umoja wa Mataifa na pia kuwepo kwake nchini humo ni kwa madhara ya wananchi wa Syria ambao wamechoshwa na vitendo vya kigaidi vya vibaraka wa Marekani kama hao magaidi wa Daesh. 

342/