Main Title

source : Parstoday
Jumatano

16 Agosti 2023

21:26:01
1387434

Onyo kuhusu ongezeko kubwa la itikadi kali za kisiasa nchini Marekani

Wakati kesi ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ikiendelea sambamba na kuandaliwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo wa mwaka 2024, wataalamu wametahadharisha kuhusu ongezeko kubwa la misimamo mikali ya kisiasa miongoni mwa Wamarekani.

Vitisho dhidi ya maafisa wa serikali ya Marekani vimekuwa vikiongezeka mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni na vimeibua changamoto mpya kwa utekelezaji wa sheria, haki za kiraia na kile kinachodaiwa kuwa ni demokrasia ya Marekani.

Kulingana na jarida la Politico la Marekani, moja ya vitisho vya hivi karibuni zaidi ni makabiliano ya mzee wa miaka 74 katika jimbo la Utah na maafisa wa Idara ya Upelelezi ya Shirikisho la Marekani (FBI). Makabiliano hayo  hatimaye yalisababisha kifo cha mzee huyo. Inasemekana mzee huyo alikuwa ametishia kwenye mtandao wa kijamii kuwa angemuua Rais Joe Biden wa Marekani .

Kwa hiyo, wataalamu wameonya kuhusu kushadidi misimamo mikali ya Wamarekani  sambamba na ongezeko la ghasia zenye muelekeo wa kisiasa.

Wiki iliyopita, mtu wa miaka 52 kutoka jimbo la Texas alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu jela kwa kutishia kuwaua wafanyikazi wa uchaguzi katika jimbo la Arizona. Siku nne kabla ya tukio hilo, waendesha mashtaka walitangaza kukamatwa kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 56 kutoka jimbo la Michigan ambaye alidanganya kuhusu kununua bunduki kwa ajili ya mtoto wake mwenye ulemavu wa akili, lakini alikusudia kuitumia dhidi ya Biden na gavana wa chama cha Democrat katika jimbo hilo. Kitengo cha Polisi katika Bunge la Marekani, Congress, kilitangaza katika ripoti yake mwaka jana kwamba idadi ya vitisho dhidi ya wabunge imeongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.Kuna mgawanyiko mkubwa wa kijamii kutokana na kuwepo kwa tofauti nyingi kati ya vyama viwili vikuu vya Marekani, yaani chama cha upinzani cha Republican na chama tawala cha Democratic, hasa kati ya Donald Trump na Joe Biden, marais wa zamani na wa sasa wa Marekani. Magwanyiko huu mkubwa unazidi kuongezeka kote Marekani . Aidha mitazamo inayokinzana mara kwa mara kuhusu masuala ya sera za ndani na nje ya Marekani, ambayo imezua taharuki katika maamuzi, sasa inadhihirika kikamilifu. Jambo hilo limesababisha ongezeko kubwa la misimamo mikali ya kisiasa na kuibuka kwa vitisho visivyo na mfano wake dhidi ya mamlaka na taasisi za shirikisho na serikali nchini Marekani. Kuongezeka migawanyiko ya ndani, haswa kati ya watu ambao hawajaridhika na serikali za majimbo na serikali ya kitaifa kumekuwa na nafasi kubwa katika kushadidisha tishio jipya la usalama, yaani, ongezeko kubwa la vitisho na vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa na watu wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Alejandro Mayorkas, Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani anasema: Misimamo mikali ya majumbani ni moja ya vitisho vikubwa vinavyohusiana na ugaidi nchini Marekani Wataalamu wa masuala ya Marekani wanasema moja ya sababu kuu za hali ya sasa ni madai yasiyothibitishwa ya rais wa zamani wa Marekani Donald Trump ambaye ameikosoa vikali FBI na pia kutilia shaka itibari ya Idara ya Mahakama ambayo imekuwa ikilaumiwa na rais huyo wa zamani tangu kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020. Sisitizo la Trump kuwa kulikuwa na wizi wa kura mbao ulipelekea Biden kushinda uchaguzi uliopita wa rais ni jambo ambalo limepelekea kuongezeka vitisho dhidi ya wafanyikazi wa uchaguzi kiasi kwamba mtu mmoja kati ya sita wanaofanya kazi katika idara ya uchaguzi wameripoti kupokea vitisho. Wakati huo huo, inasemekana kuwa wasimamizi wengi wenye uzoefu wa kuendesha zoezi la uchaguzi wameacha kazi zao au wanafikiria kuiacha.

342/