Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

17 Agosti 2023

20:15:30
1387644

Pyongyang: Askari wa US alitorokea Korea Kaskazini kutokana na ubaguzi

Serikali ya Pyongyang imesema askari Mmarekani mwenye asili ya Afrika alitorokea Korea Kaskazini kutokana na vitendo vya ubaguzi wa rangi na dhulma alizokuwa akishuhudia ndani ya jeshi la Marekani.

Kwa mujibu wa Shirika Kuu la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), Travis King ambaye aliingia Korea Kaskazini mwezi uliopita akiwa katika safari ya kitalii katika eneo linalotenganisha Korea Kaskazini na Korea Kusini, alifanya hivyo ili kukwepa madhila aliyokuwa akikumbana nayo nchini Marekani.

Taarifa ya KCNA imeeleza kuwa, askari huyo mweusi wa Marekani amekiri kuingia kinyume cha sheria nchini Korea Kaskazini akitokea Korea Kusini, lakini ameomba kupewa hifadhi ama nchini humo au katika nchi ya tatu, lakini asirejeshwa Marekani.

KCNA imeripoti kuwa: Wakati wa uchunguzi, Travis King alikiri kuwa ameamua kwenda Jamhuri ya Watu wa Korea (DPRK) ili kuondokana na vitendo visivyo vya kibinadamu na ubaguzi wa rangi alivyoshuhudia ndani ya jeshi la Marekani.

Ripoti hiyo ya  shirika la KCNA imebainisha kuwa, Travis King mwenye miaka 23 na ambaye aliingia Korea Kaskazini Julai 18, ataendelea kuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Watu wa Korea Kaskazini, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Myron Gates, mjomba ya Travis King alinukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani hivi karibuni akithibitisha kuwa, mpwa wake huyo alishuhudiwa vitendo vya kibaguzi jeshini, na alipokuwa kizuizini nchini Marekani.

342/