Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

19 Agosti 2023

20:35:07
1387964

EU yashutumiwa kwa kuwabagua wakimbizi wa Kiafrika

Umoja wa Ulaya umeendelea kukosolewa kwa kutekeleza sera za kibaguzi dhidi ya wakimbizi kutoka Ukraine kwa upande mmoja, na wale wanaotoka nchi za Afrika na bara Asia kwa upande wa pili.

Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi kwa mara nyingine tena amekosoa namna nchi za Ulaya zinavyowapokea kwa mikono miwili wakimbizi kutoka Ukraine, lakini zinawabagua na hata kukataa kuwapokea wakimbizi weusi waliotoroka vita na mapigano ya silaha katika nchi zao.

Grandi amesema, "Huu ndio ukweli unaochukiza. Wakimbizi wa Kiafrika hawapokewi vizuri (katika nchi za Ulaya) kama wanavyopokewa wakimbizi kutoka Ukraine."

Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekosoa undumakuwili huo wa nchi za Ulaya katika kuamiliana na wakimbizi wa Ukraine, na wenzao kutoka Syria, Afghanistan, Palestina, na Somalia.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema katika ripoti yake ya karibuni kwamba, idadi ya wakimbizi wanaokimbia nchi na makazi yao au watu waliolazimika kuwa wakimbizi ndani ya nchi zao haijawahi kuwa kubwa kwa kiwango kinachoshuhudiwa hivi sasa. Kwa mujibu wa shirika hilo la UN, idadi ya wakimbizi au wanaotafuta hifadhi hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana (2022) ilikuwa watu milioni 108 na laki 4. 

Muhammed Shehada, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Med Human Right Monitor amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, ubaguzi wa EU kwa wakimbizi na wahamiaji umegeuka na kuwa kitu cha kawaida siku baada ya siku. 

342/