Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

21 Agosti 2023

21:05:13
1388458

Kubariki Marekani mpango wa kuipelekea Ukraine ndege za kivita aina ya F-16

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ametangaza kuwa Washington imeafiki kupelekewa Ukraine ndege za kivita aina ya F-16 kutoka nchi mbili wanachama wa shirika la kijeshi la NATO, yaani Denmark na Uholanzi, na kwamba hilo litafanyika baada ya kukamilishwa mchakato wa utoaji mafunzo kwa marubani wa Ukraine ya kuzitumia ndege hizo.

Ukraine, ambayo tangu mwaka jana imekuwa ikishinikiza ipatiwe ndege hizo imesifu uamuzi huo uliotangazwa na Washington. Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov ameuelezea uamuzi huo wa Marekani kama "habari nzuri sana". Pamoja na hayo, inatarajiwa kuchukua miezi kadhaa mpaka Ukraine itakapoweza kuzitumia ndege za kivita za F-16 kwa ajili ya kukabiliana na uwezo wa juu wa anga ilionao Russia kwa sasa dhidi yake. Hapo awali, msemaji wa Jeshi la anga la Ukraine Yuri Ihnat alikiri kuwa Kiev haitakuwa imeweza kuziendesha ndege za F-16 ufikapo msimu ujao wa mapukutiko au wa baridi kali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Wopke Hoekstra ametangaza kuhusiana na suala hilo kuwa, nchi hiyo inakaribisha uamuzi wa Washington wa kufungua njia ya upelekaji ndege za kivita za F-16 nchini Ukraine. Hoekstra amesema: "hii ni hatua kubwa kwa Ukraine ili kuweza kulinda watu wake na nchi yake." Wizara ya ulinzi ya Denmark ilitangaza siku ya Ijumaa kwamba muungano wa mataifa 11 utaanza kutoa mafunzo kwa marubani wa Ukraine ya kurusha ndege za kivita aina ya F-16 nchini Denmark ifikapo mwisho wa mwezi huu. Waziri wa Ulinzi wa Denmark, Jakob Ellemann-Jensen amesema: "Serikali imesema mara kadhaa kwamba kuwatunuku (ndege hizi) itakuwa hatua ya kutarajiwa itakayokuja kufuatia ya utoaji mafunzo. Sasa hivi tunalijadili hilo na washirika wetu wa karibu."Kutoa baraka zake Marekani kwa mpango wa kuipatia Ukraine ndege za kivita za F-16 kunafanyika, ilhali nchi hiyo na washirika wake katika shirika la kijeshi la NATO hapo awali walikataa Ukraine kupatiwa ndege hizo. Nchi hizo zilidai kwamba hatua hiyo inaweza kupanua wigo wa vita na Russia, ambayo imejizatiti kwa silaha za nyuklia. Lakini kwa uamuzi iliochukua hivi sasa wa kuafiki ndege za kivita za F-16 zipelekwe nchini Ukraine, Marekani imechukua hatua nyingine ya kuendeleza na kushamirisha vita vya Ukraine. Ted Snider, mwandishi wa habari wa Kimarekani ameandika makala katika tovuti ya American Conservative ambayo ndani yake ameashiria juhudi zilizofanywa na nchi tatu tofauti za kuzileta kwenye meza ya mazungumzo Russia na Ukraine, ambapo pande hizo mbili zilifikia hatua ya kuridhisha ya makubaliano; na hata katika moja ya mazungumzo hayo yaliyofanyika Istanbul, Uturuki yalikaribia kusainiwa makubaliano ya suluhu kati ya pande mbili hizo hasimu, lakini Marekani iliyasimamisha mazungumzo yote hayo matatu.Kwa mtazamo wa serikali ya Biden, kushinda Russia katika vita vya Ukraine, tena mbele ya macho ya NATO, kutalidharaulisha shirika hilo la kijeshi na kupelekea kupanuka zaidi ushawishi na nguvu za Russia kikanda na kimataifa na kubadilisha mlingano wa kiusalama, kijeshi na kisiasa barani Ulaya kwa madhara ya nchi za Magharibi. Aidha, Rais Joe Biden wa Marekani na maafisa wakuu wa kijeshi na usalama wa serikali yake wanaamini kuwa, vita vya Ukraine ni fursa ya kipekee na isiyoweza kujirudia kwa ajili ya kupambana na Russia kadiri inavyowezekana na kuidhoofisha nchi hiyo ili hatimaye kuzuia kuundwa kikamilifu mfumo wa kambi kadhaa duniani. Kwa sababu hiyo, na kama wanavyodai wenyewe, wamejizatiti kuhakikisha wanaizuia Russia kushinda vita vya Ukraine kwa gharama yoyote ile. Hatua inazojaribu kuchukua Marekani ili kuendeleza vita nchini Ukraine kwa lengo la kuidhibiti na kuidhoofisha Russia zinashuhudiwa huku kukitolewa takwimu za kutisha za maafa ya roho za watu yaliyosababishwa na vita hivyo. Gazeti la Marekani la New York Times limeripoti kuwa, katika muda wa miezi 18 iliyopita tangu vilipoanza vita vya Ukraine mnamo Februari 24, 2022, karibu wanajeshi nusu milioni wa Russia na Ukraine wameuawa au kujeruhiwa katika vita hivyo.Kwa mtazamo wa Moscow, madhumuni ya Marekani ya kuendeleza vita nchini Ukraine ni kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana, lengo kuu hatimaye likiwa ni kuigawanya vipande vipande nchi hiyo. Na hilo ndilo suala ambalo Wamarekani wamekuwa wakilifuatilia tangu enzi za Shirikisho la Kisovieti la Urusi. Kwa hali hiyo, kinachotarajiwa ni kwamba vita vya Ukraine, ambavyo hadi sasa na baada ya kupita miezi 18, vimeshasababisha maafa makubwa ya roho za watu, hasara kubwa za kijeshi pamoja na kuangamiza miundombinu ya Ukraine, sio tu havitaisha, -lakini kutokana na uungwaji mkono mkubwa ambao Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine anaupata kwa Marekani na nchi nyingine za Magharibi kama ulivyotangazwa wakati wa mkutano wa hivi karibuni wa viongozi wa NATO uliofanyika nchini Lithuania-, tutarajie kushuhudia kuendelea na kupamba moto zaidi vita hivyo katika miezi ijayo pia.../