Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

21 Agosti 2023

21:05:55
1388459

Rais wa Afrika Kusini: Zaidi ya nchi 20 zimeomba kujiunga na BRICS

Zaidi ya nchi 20 zimetuma maombi rasmi ya kujiunga na BRICS, muungano wa mataifa yanayoinukia kiuchumi unaojumuisha Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.

Akihutubia taifa Jumapili usiku kwa njia ya televisheni, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema:"BRICS iliyopanuliwa itawakilisha kundi tofauti la mataifa yenye mifumo tofauti ya kisiasa ambayo ina mtazamo wa pamoja wa kuwa na utulivu wa kimataifa."

Afrika Kusini itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 15 wa wakuu wa nchi za BRICS mjini Johannesburg, ambao utahudhuriwa na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Rais Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi. Rais Vladimir Putin wa Russia atawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Sergey Lavrov.

Mwezi Machi, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati ya kukamatwa Putin, ambayo ilimzuia kusafiri kuhudhuria mkutano huo, ambao umepangwa kufanyika kuanzia Agosti 22-24.

Afrika Kusini imetia saini Mkataba wa Roma, ambao ulianzisha mahakama hiyo.

Rais Xi atawasili Afrika Kusini siku ya Jumatatu, siku moja kabla ya kuanza mkutano huo, katika ziara yake ya nne ya kiserikali nchini humo.

Afrika Kusini ina uhusiano wa kimkakati na China na inatarajiwa kusaini mikataba kadhaa wakati wa ziara ya Xi.

Ramaphosa amesema kuwa zaidi ya wakuu 30 wa nchi na serikali kutoka kote barani Afrika watahudhuria mkutano huo.

Ramaphosa amesema kuwa kando na kuwakaribisha viongozi wengine wa Afrika, pia watakuwa wakiwakaribisha viongozi kutoka mataifa kadhaa ya Ukanda wa Kusini.

Viongozi watakaofika ni kutoka maeneo ya Karibiani, Amerika ya Kusini, Asia Magharibi, Asia ya Kusini na Kusini-mashariki mwa Asia.

Amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia atahudhuria mkutano huo kufuatia mwaliko wa umoja huo.

Ramaphosa amesema nchi yake inaunga mkono upanuzi wa uanachama wa BRICS, ambao thamani yake inaenea zaidi ya maslahi ya wanachama wake wa sasa.

BRICS kwa sasa ni robo ya uchumi wa dunia, ikiwa ni sehemu ya tano ya biashara ya kimataifa, na ni nyumbani kwa zaidi ya asilimia 40 ya idadi ya watu duniani.Amesema wanataka kujenga ushirikiano kati ya BRICS na Afrika ili bara hilo liweze kufungua fursa za kuongezeka biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu.