Ugunduzi wa makaburi hayo ungali unaendelea kiasi kwamba katika
kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya makaburi 1,300 ya watoto
yamegunduliwa karibu na baadhi ya taasisi za kielimu za makanisa ambazo
zilikuwa sehemu ya mfumo wa elimu kwa ajili ya watoto wenyeji wa nchi
hiyo. Kuhusiana na suala hilo, siku ya Jumatano moja ya makabila ya
wachache ya wazawa asilia wa Canada yanayoishi magharibi mwa nchi hiyo
lilitangaza kugunduliwa kwa kaburi la umati la watoto wapatao mia moja
katika eneo hilo.
Kabila hilo la The English River First Nation limesema kwamba kilichogunduliwa kinahuzunisha sana. Kufikia sasa, makaburi 93 ambayo hayana alama yoyote yakiwemo ya watoto 79 na watoto wachanga 14 yamegunduliwa katika nchi hiyo.
Makaburi mapya yamegunduliwa kufuatia utafiti uliofanywa karibu na shule ya bweni ya wenyeji asilia inayoitwa Beauval katika eneo la Saskatchewan, Canada. Kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Regina, majengo ya shule hiyo yaliharibiwa na wakaazi baada ya kufungwa mnamo 1995.