Risasi zenye urani hafifu
zitatumiwa kwenye vifaru vya Kimarekani vya Abrams ambavyo itakabidhiwa
Ukraine na zina uwezo wa kuteketeza vifaru vya Russia. Kiev inatarajiwa
kupokea shehena ya risasi hizo katika kipindi cha wiki chache zijazo; na
japokuwa kiwango kamili cha shehena mpya ya silaha itakayopatiwa
Ukraine bado hakijafahamika, lakini silaha hizo zitagharimu dola
milioni 240 hadi 375.
Miezi michache iliyopita, Uingereza
pia ilipeleka Ukraine silaha zenye madini ya urani hafifu, lakini hii ni
mara ya kwanza kwa Marekani kuchukua hatua hiyo, na inatarajiwa kwamba
hatua hiyo ya Washington itazusha makelele. Katika hatua tatanishi
nyingine inayofanana na hiyo, Marekani tayari ilikwisha ipatia Ukraine
shehena ya mabomu ya vishada (cluster bombs) ili iyatumie katika vita na
Russia. Marekani, ikiwa ndiye kinara wa nchi za Magharibi na shirika la
kijeshi la NATO, inafanya kila iwezalo kuendeleza na kupanua wigo wa
vita vya Ukraine kwa lengo la kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana
na kuisababishia nchi hiyo maafa makubwa ya roho za watu na hasara kubwa
kwa zana zake za kijeshi. Hatua ya karibuni kabisa ya Washington katika
uga huo ni kupeleka Ukraine risasi zenye urani iliyohafifishwa. Kwa
kuzingatia mkwamo uliopo hivi sasa katika mashambulio ya kujibu mapigo
yanayofanywa na jeshi la Ukraine, hatua hiyo inachukuliwa kwa matumaini
ya kutoa vipigo vikali kwa wanajeshi wa Russia na kuwalazimisha
waondoke katika maeneo waliyoyateka. Utumiaji wa risasi zenye madini ya
urani hafifu ni miongoni mwa masuala yanayopigiwa kelele; na wapinzani
wake, ukiwemo Muungano wa Kimataifa wa Kupiga Marufuku Silaha zenye
Urani, wametangaza kuwa aina hiyo ya silaha ni hatari na husababisha
saratani au kuzaliwa watoto wenye ulemavu. Urani hafifu ni miongoni mwa
mabaki ya urani iliyorutubishwa, ambayo inapotumiwa katika risasi,
huwezesha kupenya kwa urahisi kwenye magari ya kivita na kuyateketeza
kwa haraka; lakini husababisha pia wingu linalotokana na vumbi la
chembechembe za urani ambalo lina athari mbaya kwa wanadamu, viumbe
vingine pamoja na mazingira pia. Marekani ilitumia kwa wingi risasi
zenye urani hafifu katika vita vya Ghuba ya Uajemi kwenye miaka ya 1990
na 2003. Mnamo mwaka 1999, shirika la kijeshi la NATO, nalo pia
lilitumia silaha hizo angamizi katika mashambulio dhidi ya Yugoslavia.Kwa mtazamo wa serikali ya Biden, kupata ushindi Russia katika vita
vya Ukraine, tena mbele ya macho ya NATO, kutalidharaulisha shirika
hilo la kijeshi na kupelekea kupanuka zaidi ushawishi na nguvu za Russia
kikanda na kimataifa na kubadilisha mlingano wa kiusalama, kijeshi na
kisiasa barani Ulaya kwa madhara ya nchi za Magharibi. Kwa hiyo, katika
mantiki ya serikali ya Marekani, ni jambo linalokubalika kuchukua hatua
yoyote ile itakayozuia kuthibiti kwa jambo hilo ikiwa ni pamoja na
kutumia risasi zenye urani hafifu. Aidha, Rais Joe Biden wa Marekani na
maafisa wakuu wa kijeshi na usalama wa serikali yake wanaamini kuwa,
vita vya Ukraine ni fursa ya kipekee na isiyoweza kujirudia kwa ajili ya
kupambana na Russia kadiri inavyowezekana na kuidhoofisha nchi hiyo
ili hatimaye kuzuia kukamilika mpango wa kuasisiwa mfumo wa kambi kadhaa
duniani. Kwa sababu hiyo, na kama wanavyodai wenyewe, wamejizatiti
kuhakikisha wanaizuia Russia kushinda vita vya Ukraine kwa gharama
yoyote ile.Kwa mtazamo wa Moscow, madhumuni ya
Marekani ya kuendeleza vita nchini Ukraine ni kuidhoofisha Russia
kadiri inavyowezekana, lengo kuu hatimaye, likiwa ni kuigawanya vipande
vipande nchi hiyo. Kauli ya karibuni zaidi iliyotolewa kuhusiana na
suala hilo ni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony
Blinken aliyedokeza kuwa ni asilimia tano tu ya bajeti ya ulinzi ya
Marekani inatumika kwa ajili kuipatia Ukraine misaada ya kijeshi na
silaha. Blinken ameendelea kusema: "sasa hivi tunalidhoofisha na
kuliangamiza jeshi la Russia kwa gharama ndogo mno ikilinganishwa na
gharama za matumizi yetu mengine ya kijeshi. Ni jambo zuri kuwepo Russia
iliyodhoofishwa".
342/