Main Title

source : Parstoday
Jumapili

3 Septemba 2023

18:12:48
1390904

Russia yaweka tayari makombora ya nyuklia yatakayomfanya adui afikirie mara mbili

Russia imetangaza kuwa imeweka tayari makombora yake ya nyuklia, ambayo Rais Vladimir Putin aliwahi kusema kuwa yatawafanya maadui wa nchi hiyo "kufikiria mara mbili" kuhusu vitisho vyao.

Mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Russia  la Roscosmos ametangaza kuwa nchi hiyo imeyatuma makombora ya masafa marefu ya Sarmat "kwenye eneo la mapigano".

Mkuu wa Roscosmos Yuri Borisov amefichua kuwa, "Mfumo wa kimkakati wa Sarmat umechukua mkao wa tahadhari ya mapigano."

Kombora Sarmat, ambalo uundwaji wake ulitangazwa mnamo 2018, limewahi kuonyeshwa mara kadhaa katika magwaride ya kijeshi mjini Moscow.

Katika hotuba ya kufichua kombora la Balistiki la Baina ya Mabara (ICBM) mnamo Machi 2018, Putin alipongeza safu ya silaha mpya za kisasa ambazo alisema zinaweza kufanya mfumo wa kuzuia makombora wa Marekani "kutofanya kazi". Putin alisema kwa yakini kuwa Sarmat ni "silaha ya kipekee."

Kombora la RS-28 Sarmat lina uwezo wa kubeba kwa uchache vichwa 10 vya nyuklia na linakusudiwa kuchukua nafasi ya  makombora ya ICBM ya R-36.

Russia imesema kuwa mfumo huu wa makombora unaweza kushambulia hadi ncha za Kaskazini au Kusini za sayari ya dunia.

Kulingana na makadirio ya wataalamu, RS-28 Sarmat lina uwezo wa kubebe  kichwa cha kivita cha MIRVed chenye uzito wa hadi tani 10 kwenye eneo lolote duniani.Hayo yanaripotiwa siku chache baada ya Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa kusema kwamba: "Russia imetahadharisha mara kadhaa na kila wakati kwamba hali ni ya hatari mno na kuna hatari ya kutokea mapigano ya moja kwa moja kati ya Russia na NATO."

Hadi sasa, shirika la kijeshi la NATO na waungaji mkono wengine wa Ukraine wa Kimagharibi wameshatuma zaidi ya dola bilioni 160 za msaada wa kijeshi na silaha kwa nchi hiyo na wamelazimika kupokea mamilioni ya wakimbizi na wahasiriwa wa vita vya Ukraine katika nchi zao.

Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameendelea kueleza kwamba NATO "imejiingiza mno katika vita vya Ukraine" na hakuna uhakika kwamba mbali na silaha na vifaa, nchi za Magharibi hazitumi majeshi yao huko Ukraine na kushiriki katika operesheni maalumu.

Vita vya Ukraine vilianza kutokana na nchi za Magharibi kutozingatia matakwa ya kiusalama ya Moscow na upanuzi wa vikosi vya NATO hadi karibu na mipaka ya Russia.

342/