Main Title

source : Parstoday
Jumatatu

4 Septemba 2023

18:52:22
1391170

Jenerali Brice Oligui Nguema aapishwa kuwa rais wa mpito wa Gabon

Jenerali Brice Oligui Nguema, ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoung'oa madarakani utawala wa makumi ya miaka wa familia ya Bongo, ameapishwa leo Jumatatu kuwa "rais wa serikali ya mpito" ya Gabon.

Taarifa kutoka nchini Gabon zinasema kuwa, sherehe rasmi za kuapishwa Nguema zimefanyika kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Libreville katika ikulu ya rais inayojulikana kwa jina la "Renovation Palace."

Katika sehemu moja ya kiapo chake mbele ya majaji wa Mahakama ya Katiba, Nguema amesema: "Ninaapa kuwa nitajitolea kwa dhati na kwa heshima kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunafikia kwenye umoja wa kitaifa. 

Jumatano iliyopita kundi moja la kijeshi lililoongozwa na Jenerali Brice Oligui Nguema liliupindua utawala wa miaka 55 wa familia ya Bongo na kubatilisha matokeo ya uchaguzi na kuvunja taasisi za serikali.

Baada ya hapo wanajeshi waliofanya mapinduzi walimteua Nguema kuwa mkuu wa kipindi cha mpito na kusimamia mchakato wa uchaguzi na kurejesha demokrasia na utawala wa Katiba nchini humo. 

Jenerali Nguema alikuwa mkuu wa walinzi wa rais na msaidizi wa familia ya Bongo iliyotawala Gabon tangu mwaka 1967. 

Rais Ali Bongo Ondimba, alipinduliwa na wanajeshi siku ya Jumatano, muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita, matokeo ambayo yalikataliwa na wapinzani waliosema ni udanganyifu mtupu. 

Katika sehemu nyingine ya kiapo chake cha leo Jumatatu, Nguema amesema: "Ninaapa mbele ya Mungu na watu wa Gabon kwamba nitalinda kwa uaminifu utawala wa Jamhuri."

Hapo hapo ameahidi kuitisha chaguzi huru na za wazi baada ya kipindi cha mpito lakini hakusema kipindi hicho cha mpito kitaisha mwaka gani.

342/