Main Title

source : Parstoday
Jumanne

5 Septemba 2023

13:14:06
1391406

Kuendelea vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi

Katika muendelezo wa siasa za chuki na propaganda chafu dhidi ya Uislamu (islamophobia) katika nchi za Magharibi, polisi ya Sweden imewatia mbaroni watu 15 kwa kujaribu kuzuia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Salwan Momika, mkazi wa Sweden ambaye katika kipindi cha miezi kadhaa ya hivi karibuni ameivunjia heshima Qur’ani mara kadhaa akitekeleza vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Uislamu; mara hii kafiri huyo akiwa katika kitongoji cha Varnhemstorget chenye wakazi wengi Waislamu ameivunjia heshima Qur’ani Tukufu. Hata hivyo hatua yake hiyo ilikabiliwa na malalamiko na upinzani wa wakazi wengi wa eneo hilo ambapo zaidi ya watu 100 walimrushia mawe na chupa za maji.

Baada ya kushadidi malalalamiko hayo, polisi ya Sweden iliingilia kati na kumuunga mkono Momika sambamba na kuwatia mbaroni zaidi ya waandamanaji 15.

Katika miezi ya hivi karibuni, nchi za Sweden na Denmark, zikitumia kisingizio cha madai yao ya "uhuru wa kujieleza", zimetoa vibali vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kwa watu wenye misimamo mikali, na kwa hakika, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu vimekuwa vikiendelea kufanyika katika mataifa hayo mawili kwa baraka kamili na uungaji mkono wa serikali za mataifa hayo yaliyoko katika bara la Ulaya.

Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vinaendelea kushuhudiwa katika mataifa ya Magharibi katika hali ambayo, nchi hizo daima zimekuwa zikitoa madai ya uhuru wa kujieleza.  

Ukweli wa mambo ni kuwa, madola ya Magharibi yamekuwa yakipuuza kwa makusudi tofauti iliyopo baina ya uhuru wa kujieleza na kutusi au kuvunjia heshima matukufu ya dini. Madola ya Magharibi yamekuwa yakitoa vibali hitajika kwa ajili ya ajili ya kuchoma moto Qur’ani na wakati huo huo kumuunga mkono mtu anayevunjia heshima Qur’ani kwa kisingizio cha uhuru wa kusema au uhuru wa kutoa maoni katika hali ambayo, inawashambulia, kuwapiga au hata kuwatia mbaroni watu wanaolalamikia vitendo kama hivi. Je uhuru huu upo tu katika kuvunjia heshima matukufu ya dini lakini watu ambao dini yao inavunjiwa heshima hawana uhuru wa kulalamika na kupinga hilo katika fremu ya kutoa maoni?

Ukweli wa mambo ni kuwa, tukitupia jicho vigezo vya kindumakuwili vya madola Magharibi zikiwemo Sweden na Denmark kuhusiana na uhuru wa kutoa maoni tunaona kuwa, msamiati wa 'uhuru wa kutoa maoni" hubeba maana pale tu unapohoji na kuvunjia heshima jambo ambalo ndio mtazamo wa Magharibi kama vile chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu. Lakini mambo ni kinyume kabisa kuhusiana na masuala mengine kama ngano ya Holocaust na kadhalika.

Tobias Billstrom, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sweden hivi karibuni alikiri kwamba kufanya mambo dhidi ya Uislamu ni jambo la kutisha na kusema kuwa Stockholm inataka kuimarisha uhusiano na nchi za Kiislamu. Vile vile alidai kuwa, nchi hiyo inapinga vikali kitendo chochote cha chuki dhidi ya Uislamu na kuvunjia heshima Qur’an au kitabu chochote kitakatifu na kitendo hicho kinahesabiwa kuwa udhalilishaji na kuvunjia heshima.

Licha ya masikitiko hayo yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa Swden, lakini serikali ya nchi hiyo inadai kuwa, kwa mujibu wa sheria maalumu za kulinda uhuru wa kujieleza haiwezi kuzuia kitendo hiki.

Chuki dhidi ya Uislamu na mfano wake wa wazi ni kuchomwa moto Qur'ani Tukufu katika nchi za Ulaya sambamba na sera nyinginezo kama vile kufungua kesi za kubambikiza dhidi ya Waislamu, kutusi na kudhalilisha matukufu ya Kiislamu, propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu pamoja na ubaguzi wa aina mbalimbali dhidi yao na hata kutishiwa kupokonywa uraia ni mambo ambayo kivitendo yamepelekea Waislamu wawe chini ya mashinikizo maradufu ya kisiasa na kijamii, jambo ambalo ni kinyume kabisa na madai ya uhuru yanayopigiwa upatu katika nchi za Magharibi.

Farhan Haqq, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa sanjari na kuashiria kwamba, kitendo cha kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu ni kibaya, kisichokubalika na cha utovu wa adabu dhidi ya Waislamu amesisitiza umuhimu wa kulindwa uhuru wa kusema kama haki ya kimsingi ya mwanadamu na kubainisha kwamba, kuvunjia heshima vitabu vitakatifu, maeneo ya ibada na nembo za kidini ni jambo ambalo halikubaliki kabisa.

Undumakuwili wa madola ya Magharibi haukomei tu katika suala hili. Mfano mwingine wa wazi ni vita vya Ukraine na Russia ambapo wanaotoa maoni na mitazamo kuhusu vita hivyo ambayo ni kinyume na mtazamo wa madola ya Magharibi wanakabiliwa na mashinikizo ya kila upande na wakati mwingine wanafuatiliwa na hata kushtakiwa.

342/