Main Title

source : Parstoday
Jumatano

6 Septemba 2023

13:18:14
1391627

Makumi ya wanafunzi wa kike Waislamu Ufaransa warejeshwa majumbani kwa kuvaa abaya

Katika siku ya kwanza ya mwaka wa masomo, skuli za umma nchini Ufaransa zimewarejesha majumbani wasichana kadhaa kwa kukataa kuvua mabaibui ya abaya yanayovaliwa na baadhi ya wanawake na wasichana wa Kiislamu. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Gabriel Attal.

Attal amevieleza vyombo vya habari kuwa, wasichana Waislamu wapatao 300 walifika maskulini mwao siku ya Jumatatu wakiwa wamevaa vazi hilo, wakikaidi marufuku iliyowekwa na serikali kwa kisingizio kwamba vazi la abaya ni nembo ya kidini.

Kwa mujibu wa waziri wa elimu wa Ufaransa, akthari ya wanafunzi hao walikubali kuvua vazi hilo, lakini 67 kati yao hawakuwa tayari kufanya hivyo; na kwa hiyo wakarejeshwa nyumbani.

Serikali ya Paris ilitangaza mwezi uliopita kuwa inapiga marufuku baibui la abaya maskulini, ikidai kuwa eti linakiuka sheria za mfumo wa Usekulari katika sekta ya elimu ambapo tayari mtandio wa kichwa, maarufu kama hijabu, umepigwa marufuku kwa madai kuwa unaashiria mfungamano wa kidini.

Jumuiya inayowakilisha Waislamu nchini Ufaransa iitwayo Action for the Rights of Muslims (ADM) imewasilisha ombi la malalamiko dhidi ya mamlaka za serikali kwa Baraza la Utawala, ambayo ni mahakama ya juu zaidi ya nchi hiyo kupinga marufuku ya vazi la abaya na qamis au kanzu, vazi linalovaliwa na Waislamu wanaume.

Hoja ya ADM ilitarajiwa kusikilizwa jana Jumanne.

Mnamo mwaka 2004 serikali ya Ufaransa ilipiga marufuku wasichana kuvaa mitandio hasa katika shule zinazomilikiwa na serikali. Abaya, ambalo linachukuliwa kuwa buibui la mtindo wa kisasa huvaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu kama vazi la stara pamoja na mtandio wa kichwa kukamilisha vazi la Hijabu.

Tangu Emmanuel Macron alipingia madarakani kushika hatamu za urais nchini Ufaransa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kuvunjiwa heshima matukufu ya  Uislamu vimeongezeka mno katika nchi hiyo ya Ulaya.../

342/