Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilitangaza jana
Jumatano kwamba: Marekani itaipa Ukraine risasi za mizinga zenye madini
ya urani hafifu ikiwa ni sehemu ya shehena mpya ya msaada wenye thamani
ya dola milioni 175.
Baada ya kuthibitishwa ripoti za kutumwa shehena ya risasi za
vifaru zenye urani hafifu, Farhan Haq, naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa
alitangaza hapo jana kuwa, Umoja wa Mataifa umekuwa na wasiwasi kila
mara juu ya kutumiwa risasi zenye urani hafifu katika sehemu yoyote ya
dunia.
Haq alisema: "wasiwasi wetu kuhusu utumiwaji wa urani hafifu katika sehemu yoyote duniani ni thabiti na ungali upo palepale".
Kabla ya hapo, shirika la habari la Reuters iliripoti kuwa kwa mara
ya kwanza, utawala wa Joe Biden utaipatia Ukraine risasi zenye urani
iliyohafifishwa.
Utumiaji wa risasi zenye madini ya urani hafifu ni miongoni mwa masuala yanayopigiwa kelele; na wapinzani wake, ukiwemo Muungano wa Kimataifa wa Kupiga Marufuku Silaha zenye Urani, wametangaza kuwa aina hiyo ya silaha ni hatari na husababisha saratani au kuzaliwa watoto wenye ulemavu.
Marekani ilitumia kwa wingi risasi zenye urani hafifu katika vita vya Ghuba ya Uajemi kwenye miaka ya 1990 na 2003. Mnamo mwaka 1999, shirika la kijeshi la NATO, nalo pia lilitumia silaha hizo angamizi katika mashambulio dhidi ya Yugoslavia. Uzoefu wa vita umeonyesha kuwa, kama yalivyo mabomu ya vishada, risasi zenye urani iliyohafifishwa huua zaidi raia kuliko askari.../
342/