Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

7 Septemba 2023

15:15:05
1391908

Sheikh Ibrahim Zakzaki: Muqawama wa Imam Husain AS ndiyo njia pekee ya kuokoka mwanadamu

Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, kuendeleza njia ya Imam Husain AS ndilo chaguo pekee bora la kuweza kumwokoa mwanadamu mbele ya dhulma na ukandamizaji.

Sheikh Ibrahim Zakzaki amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na shirika la habari la Iran Press mjini Abuja na kuongeza kuhusu umuhimu wa ujumbe wa maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS kwamba, kujitolea muhanga mtukufu huyo na Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu SAW na wafuasi wao watiifu katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria, ni muhimu sana kwa ajili ya kufikia ushindi wa uadilifu na wa haki dhidi ya dhulma na ukandamizaji duniani na njia pekee ya kuweza kuokoka mwanadamu ni kuendeleza muqawama kama wa Imam Husain AS.

Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria vile vile ametoa mkono wa pole kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa umma mzima wa Kiislamu kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Husain AS.

Amesisisitiza kuwa, watu wa zama hizi wanahitajia mno kujitolea katika njia ya haki kama alivyojitolea Imam Husain AS na wafuasi wake katika jangwa la Karbala mwezi 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

Athari za muqawama na mapambano ya Imam Husain AS zimebakia hai hadi leo na zitabakia milele hadi mwisho wa dunia. Imam Husain AS alimwaga damu yake katika njia ya ukombozi na kuwa kigezo bora kwa kila mpigania ukombozi duniani awe Muislamu na hata wasio Waislamu.

Sheikh Ibrahim Zakzaki ameongeza kuwa, kitu ambacho Imam Husain AS alikipigania na kuwaga damu yake kwa ajili yake kuna siku kitatimia tu na hicho si kitu kingine ghairi ya ushindi kamili wa uadilifu na haki dhidi ya dhulma. 

342/