Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

8 Septemba 2023

10:47:36
1392086

Guterres: Dunia inakabiliwa na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, dunia inakabiliwa na mgogoro wa mabadiliko ya tabia nchi.

Antonio Guterres ameyasema hayo katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya ASEAN HUKO Jakarta mji mkuu wa Indonesia.

Katika mkutano huo wa Jumuiya ya Mataifa ya kusini mashariki mwa Asia unaofanyika mjini Jakarta, Guterres amewataka viongozi wa jumuiya hiyo wachukue hatua kupunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuunga mkono maendeleo ya kijani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, miezi ya Juni, Julai na Agosti ilivunja rekodi kwa kuwa yenye joto kali na na kwamba hali hiyo inaonesha haja ya kuongeza nguvu ya pamoja na mshikamano katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mgogoro mbaya zaidi wa mabadiliko ya tabianchi bado unaweza kuepukika lakini muda unayoyoma hivyo haipaswi kuendelea kuupoteza.

Guterres amesema hayo katika hotuba yake mbele ya viongozi wa nchi 10 zinazounda Jumuiya ya ASEAN pamoja na wawakilishi wa mataifa ya Korea Kusini, Marekani, Japan, China, Russia, India, Australia na New Zealand.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amependekeza kuwepo kwa kile alichokiita "Mkataba wa Pamoja wa hali ya hewa" ambapo mataifa yanayotoa kiwango kikubwa cha gesi chafu yatafanya juhudi za ziada kupunguza hewa hiyo, na kwa mataifa tajiri yatahamasisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha na kiufundi ili kuunga mkono nchi zenye uchumi unaoinukia.

Kwa uapnde wake Rais wa Indonesia Joko Widodo ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amewatolea mwito viongozi wa dunia kutatua mizozo inayoendelea wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN.

342/