Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

8 Septemba 2023

10:53:03
1392094

Polisi ya Rwanda yamtia mbaroni mshukiwa sugu wa mauaji

Polisi nchini Rwanda imemtia mbaroni mshukiwa wa mauaji mwenye umri wa miaka 34 ambaye anadaiwa kuua na kuzika zaidi ya miili 10 jikoni kwake.

Polisi waligundua kuhusu mauaji hayo baada ya kumfukuza mwanamume huyo kutoka katika nyumba yake ya kukodi katika wilaya ya Kicukiro, kitongoji cha mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Mwenye nyumba wake alikuwa amewataka wafanye hivyo kwa vile alikuwa amekosa kulipa kodi kwa miezi saba iliyopita.

Afisa wa polisi aliliambia gazeti binafsi la Rwanda la The New Times kwamba walipokwenda kumuondoa aliomba radhi na kulia kupita kiasi jambo ambalo liliibua mashaka yetu, tulimshikilia na mimi binafsi nilimpeleka polisi, ni kituo cha polisi ambapo alikiri kuwaua baadhi ya watu hali iliyosababisha RIB [Rwanda Investigation Bureau] kufanya uchunguzi wa makazi yake.” afisa huyo alisema.

Polisi walisema kuwa mwanamume huyo alikiri kuwarubuni waathiriwa wake kutoka kwenye baa na kisha kuwaibia, kuwaua na kuwazika kwenye shimo alilochimba jikoni kwake. Pia alifichua kuwa aliwayeyusha baadhi ya waathiriwa kwa tindikali.

Waathiriwa walikuwa wanaume na wanawake, alisema Thierry Murangira, msemaji wa Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda.

Ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanawake wanaouza miili yao ndio hasa walilengwa.

Mamlaka ilisema kuwa ilimkamata mwanamume huyo mwezi Julai kwa madai ya kuwaibia, kuwabaka na kuwatishia baadhi ya wanawake, lakini wakamwachia kwa kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha.

Chanzo cha polisi ambacho hakikutajwa jina kiliiambia AFP kwamba walikuwa wameopoa miili 14, lakini Bw Murangira alisema kuwa polisi bado wanachunguza idadi ya waathiriwa.

342/