Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Septemba 2023

20:28:30
1392470

Kupungua uzalishaji wa viwanda nchini Ujerumani; sababu na matokeo yake

Wizara ya Uchumi na Teknolojia ya Ujerumani imeripoti kwamba uzalishaji wa viwanda nchini Julai iliyopita ulishuka kwa kasi kuliko ilivyotarajiwa, na hivyo kuweka wazi matatizo yanayoukabili uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya.

Habari hii imetangazwa katika hali ambayo wachambuzi walioshiriki katika uchunguzi wa maoni wa tovuti ya DailyFX walitarajia kiwango hicho kupungua kwa nusu asilimia kila mwezi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, utafiti uliofanywa na taasisi moja ya uchunguzi wa maoni ulionyesha kuwa nusu ya wananchi wa Ujerumani, wana wasiwasi mkubwa kuhusu kudorora uchumi wa nchi yao kutokana na mwenendo wa sasa wa siasa za serikali ya Berlin, athari za vikwazo dhidi ya Russia, mfumuko wa bei na kupungua ustawi wa uchumi wa kimataifa.

Pia, kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa, mnamo Mei 2022, Ujerumani iliripoti nakisi ya biashara ya nje ambayo ilifikia euro bilioni moja. Nchi hii ilikuwa imebadilika kutoka kwenye ziada ya biashara na kuingia katika mkondo wa kuagiza zaidi bidhaa, katika muda mfupi. Bila shaka, uchumi wa Ujerumani kwa mara nyingine umepata ziada ya kibiashara mwaka huu, lakini pamoja na hayo masuala haya yanaonyesha kuwa hali ya uchumi huo mkubwa zaidi barani Ulaya si nzuri sana.

Hans-Werner Sinn, mwanauchumi mkuu wa Ujerumani, anaamini kwamba hali ya uchumi wa Ujerumani, ambayo sasa imeanza tena kuitwa "Mgonjwa wa Ulaya", ndiyo imechochea kuenea fikra za mirengo ya kulia iliyopindukia mipaka. Kulingana naye, changamoto zinazoikabili Ujerumani, kwa sasa hasa kuhusu suala la nishati, zinaweza kuvinufaisha pakubwa kisiasa vyama vya mrengo wa kulia.

Lakabu ya "Mgonjwa wa Ulaya" imeibuka tena katika wiki za hivi karibuni kutokana na uzalishaji wa viwanda vya Ujerumani, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi katika eneo la sarafu ya euro, kupungua sana, na hilo kimsingi linatokana na nchi hiyo kukabiliwa na tatizo la bei ya juu ya nishati. Lakabu hiyo ilitumika kwa mara ya kwanza kuhusu uchumi wa Ujerumani mnamo 1998, ambapo nchi hiyo ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha changamoto za gharama kubwa za kiuchumi baada ya kuunganishwa tena Ujerumani Mashariki na Magharibi.

Ingawa kuna sababu nyingi ambazo zimechangia hali mbaya ya kiuchumi ya Ujerumani katika miaka miwili iliyopita, lakini bila shaka siasa na hatua za serikali ya muungano ya Berlin dhidi ya Russia na kushiriki nchi hiyo katika vikwazo vya Magharibi dhidi ya Moscow, hasa baada ya kuzuka vita vya Ukraine na sera za kutotegemea gesi ya Russia zinachukuliwa kuwa moja ya sababu kuu ambazo zimeibua masaibu ya kiuchumi yanayoikabili Ujerumani hivi sasa.

Kwa sasa, uchumi wa Ujerumani ambao ni uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya na uchumi wa nne kwa ukubwa duniani, umeingia kwenye mdororo ambao umeibua uvumi kwamba athari zake mbaya zinaweza pia kuharibu uchumi na uzalishaji wa viwanda katika Umoja wa Ulaya na bara zima la Ulaya. Kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Shirikisho la Ujerumani, uchumi wa nchi hiyo uliingia katika mdororo katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Hiki ni kisa cha kwanza cha mdororo wa kiuchumi nchini Ujerumani tangu janga la corona, hali iliyosababisha pato la taifa kupungua katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka huo wa 2020. Takwimu mpya rasmi zinaonyesha kuwa uchumi wa Ujerumani uko katika hali mbaya zaidi kuliko makadirio ya hapo awali. Kwa hakika, uchumi huo mkubwa zaidi barani Ulaya umedorora katika robo mbili mfululizo, jambo ambalo limeibua wasi wasi mkubwa miongoni mwa wanauchumi na raia wa kawaida wa nchi hiyo.

Sababu kuu ya kudorora uchumi wa Ujerumani ni kuvurugika uhusiano wa nishati kati ya Ujerumani na Russia kufuatia vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia na kulipuliwa mabomba ya kusafirisha gesi ya Nord Stream.

Gunnar Beck, mjumbe wa Bunge la Ulaya wa chama cha "Mbadala kwa ajili ya Ujerumani", anatoa sababu nyingine za kudorora uchumi wa Ujerumani. Anasema kuwa serikali ya nchi hiyo inatekeleza siasa zisizo za busara katika uwanja wa nishati. Anaendelea kusema kwamba serikali ya Olaf Schultz Kansela wa Ujerumani, inaendelea kuongeza machungu ya kupungua uagizaji wa nishati kutoka Russia, ambayo yanaweza kufanya kudorora uchumi wa nchi hiyo kuwa mbaya zaidi.

Kwa kutilia maanani kuwa Ujerumani kwa muda mrefu, imekuwa kinara na injini inayoendesha uchumi wa Umoja wa Ulaya, matokeo ya kuharibika uchumi wa nchi hiyo yamekuwa na athari mbaya sana kwa nchi zingine za Umoja wa Ulaya kwa maana kwamba yameathiri pia uchumi wa nchi hizo.

342/