Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Septemba 2023

20:31:46
1392472

Mahakama ya Ufaransa yaidhinisha marufuku ya abaya katika skuli za nchi hiyo

Mahakama ya Ufaransa imeidhinisha marufuku ya uvaaji vazi la abaya kwa wanafunzi Waislamu wanawake katika skuli za nchi hiyo.

Baraza la Utawala, ambayo ni mahakama ya juu zaidi ya nchi hiyo imesema uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku vazi la Kiislamu la abaya maskulini umeendana na sheria ya Ufaransa, ambayo hairuhusu matumizi ya alama za kidini maskulini.

Uamuzi huo umetolewa kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Jumuiya inayowakilisha Waislamu nchini Ufaransa iitwayo Action for the Rights of Muslims (ADM) kupinga marufuku ya vazi la abaya na qamis au kanzu, vazi linalovaliwa na Waislamu wanaume iliyopitishwa na serikali ya nchi hiyo.

Marufuku ya uvaaji wa abaya katika skuli za Ufaransa ilianza kutekelezwa siku ya Jumatatu, sambamba na kuanza mwaka mpya wa masomo nchini humo.

Kwa mujibu wa waziri wa elimu wa Ufaransa Gabriel Attal wasichana Waislamu wapatao 300 walifika maskulini mwao siku hiyo wakiwa wamevaa vazi hilo kukaidi marufuku iliyowekwa na serikali kwa kisingizio kwamba vazi la abaya ni nembo ya kidini.

Wakati akthari ya wanafunzi hao walikubali kuvua vazi hilo, 67 miongoni mwao hawakuwa tayari kufanya hivyo; na kwa hiyo wakarejeshwa nyumbani.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Ufaransa, zimekuwa zikitekeleza sera za uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu katika nyanja mbalimbali za kisiasa na kijamii.   Kabla ya marufuku ya abaya, mnamo mwaka 2004 serikali ya Ufaransa ilipiga marufuku wasichana kuvaa mitandio ya kichwa hasa katika skuli zinazomilikiwa na serikali. Abaya, ambalo linachukuliwa kuwa buibui la mtindo wa kisasa huvaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu kama vazi la stara pamoja na mtandio wa kichwa kukamilisha vazi la Hijabu.../  

342/