Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Septemba 2023

20:37:28
1392478

Zaidi ya watu 1000 waaga dunia katika tetemeko la ardhi nchini Morocco

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco imetangaza kuwa, takriban watu 820 wamefariki dunia na mamia ya wengine wamejeruhiwa katika tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo usiku wa kuamkia leo Jumamosi.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco inaendelea kutoa takwimu za mara kwa mara kuhusu tetemeko hilo kubwa la ardhi huku ikiendelea kusema kuwa idadi ya wahanga wa janga hilo la kimaumbile itaongezeka kutokana na idadi kubwa ya watu kubakia chini ya vifusi.

Mtetemeko huo wa ardhi umeripotiwa kutokea katika mji wa kitalii wa Marrakech, ulioko umbali wa kilomita 320 kusini mwa mji mkuu Rabat. Zilizala hiyo yenye ukubwa wa 6.8 kwa kipimo cha rishta limeikumbwa Morocco jana usiku na kitovu chake kililikuwa ni cha kina cha kilomita 18.5 chini ya ardhi karibu na mji wa kitalii wa Marrakesh.

Tetemeko hilo la ardhi limesikika katika maeneo na miji mingi ya Morocco, ikiwemo ya Rabat na Casablanca ambalo ndilo jiji kubwa zaidi katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Noureddine Bazine, mwandishi wa habari ambaye pia ni mkazi wa eneo la Marrakesh, amesema kwamba tetemeko hilo lilikuwa la "ghafla na janga kubwa" kwa wakaazi wa jiji hilo.

“Tumepitisha usiku wa kutisha uliojaa majinamizi na ndoto mbaya; hatujazoea majanga ya aina hii,” amesema na kuongeza kuwa idadi kubwa zaidi ya vifo itaripotiwa katika eneo la al-Haous.

Pia amesema: "Huko Marrakesh, uharibifu mkubwa zaidi ulikuwa katika mji wa zamani, na kuna uwezekano majengo zaidi ya kuporomoka, na baadhi yake yanaweza kuporomoka hata bila tetemeko la ardhi kwa sababu tangu zamani ni majengo dhaifu. "Idadi ya vifo huenda ikaongezeka zaidi." 

342/