Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

9 Septemba 2023

20:39:22
1392481

Rais Museveni: Jeshi la Uganda limeangamiza mamia ya wapiganaji wa kundi la waasi la ADF

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda ametangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeua kwa akali wapiganaji 560 wa kundi la kigaidi la ADF.

Tangazo hilo linakuja majuma machache tu baada ya Meja Jenerali Dick Olum, Kamanda wa Operesheni Shujaa iliyoanzishwa na majeshi ya nchi hizo mbili jirani mnamo Novemba 31 mwaka 2021 kutangaza katikati ya mwezi uliopita wa Agosti kwamba, mamia ya waasi wa kundi linalojiita Allied Democratic Forces (ADF) wameuawa tangu vikosi vya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vianzishe Operesheni ya Shujaa dhidi ya genge hilo mashariki ya Kongo.

Kundi linaloipinga Kampala la Allied Democratic Forces (ADF) liko katika misitu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako linafanya mashambulizi ndani ya Congo na Uganda.

Baada ya kupata kibali cha Congo, wanajeshi wa Uganda walianzisha operesheni huko dhidi ya ADF wakitaka kuharibu kambi zao na kuua au kuwakamata wapiganaji wa kundi hilo.

Hata hivyo kwa ujumla mashambulizi katika maeneo hayo yamepungua kwa kiasi kukubwa, hasa katika maeneo ambayo vikosi vya pamoja vya DRC na Uganda vimekita kambi.

Waasi wa ADF wamekuwa wakiendesha harakati zao kwenye misitu mashariki mwa Kongo DR kwa zaidi ya miongo miwili sasa na wamekuwa wakifanya mashambulizi ndani ya nchi hiyo na wakati mwingine ndani ya ardhi ya Uganda. Kundi la kigaidi la DAESH limelitangaza kundi la ADF kuwa ni tawi lake katika eneo la Afrika ya Kati.

342/