Main Title

source : Parstoday
Jumapili

10 Septemba 2023

18:57:04
1392704

Russia yatungua droni 8 za Ukraine karibu na Crimea

Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imefanikiwa kutungua ndege nane zisizo na rubani (droni) za Ukraine zilizokuwa zinaruka katika anga ya Bahari Nyeusi karibu na eneo la Crimea.

Shirika la habari la Sputnik leo Jumapili limenukuu taarifa ya wizara hiyo ikisema kuwa, "Usiku wa kuamkia leo Septemba 10, jaribio la utawala wa Kiev la kufanya shambulizi la kigaidi kwa kutumia UAV (droni) katika maeneo ya Shirikisho la Russia limetubuliwa."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Mifumo ya ulinzi wa anga  (ya Russia) imesambaratisha ndege nane zisizo na rubani katika anga ya Bahari Nyeusi karibu na pwani ya Jamhuri ya Crimea.

Aidha Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema boti tatu za kijeshi za Kimarekani zilizokuwa zimebeba askari wa Ukraine zimeharibiwa kaskazini mwa Kisiwa cha Nyoka pwani ya Bahari Nyeusi.

Juzi Ijumaa pia, jeshi la nchi hiyo lilizima mashambulio 21 ya Ukraine na kuua takriban wanajeshi 630 wa serikali kibaraka ya Kiev katika maeneo ya Donetsk, Kupyansk, Zaporozhye, Krasnyi Lyman na Kherson.

Kadhalika mwezi uliopita, Russia kupitia vita vya kielektroniki ilitungua ndege 11 zisizo na rubani za Ukraine karibu na eneo la Crimea, na nyingine mbili zilizokuwa zinaelekea Moscow.

Russia imekuwa ikisisitiza kuwa, shambulio lolote la Ukraine dhidi ya eneo la Crimea litaiepelekea Moscow kutumia 'silaha za aina yoyote' kujibu mapigo na kujilinda.

342/