Main Title

source : Parstoday
Jumapili

10 Septemba 2023

19:39:04
1392716

Waislamu Ghana wafanya matembezi ya amani kuadhimisha Arubaini

Maelfu ya Waislamu ya madhehebu ya Shia nchini Ghana wamefanya matembezi ya amani ya kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein (AS).

Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, matembezi hayo ya kumbukumbu ya Arubaini ya mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, aliyeuawa kidhulma katika jangwa la Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria yamefanyika Accra, mji mkuu wa Ghana.

Iran Press imeripoti kuwa, wanaume, wanawake na watoto waliokuwa wamevalia mavazi meusi walifanya matembezi hayo jana Jumamosi kuanzia Ofisi ya Waislamu wa Kishia ya Maamobi hadi katikati ya Accra, katika Ofisi Kuu ya Mashia mjini hapo. 

Mmoja wa washiriki wa matembezi hayo, Memuna Sadat Banda amesema, "Mtume Muhammad SAW alilizwa na tukio hili chungu la kuuawa kidhulma Imam Hussein AS, hivyo ni wajibu kwa kila Muislamu kuguswa na kuhuzunishwa na siku hii."

Katibu wa Jumuiya ya Majma Ahlul Bayt, Muhammed Kabir ambaye ameashiriki matembezi hayo jijini Accra ameiambia Iran Press kuwa, matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS si tu ni tukio la kihistoria, lakini pia ni tukio la kidini lenye umuhimu mkubwa.

Vikao, marasimu na matembezi ya tukio la kila mwaka ambalo linaadhimisha siku ya 40 baada ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), Imam wa tatu wa kizazi cha Ahlul Bayt AS yamekuwa yakifanyika tokea Jumatano katika pembe mbalimbali za dunia zikiwemo nchi za Afrika.

Jumatano iliyopita, Waislamu ya madhehebu ya Shia nchini Nigeria walifanya matembezi na vikao vya kuadhimisha kumbukumbu hiyo katika mji wa Suleja, jimbo la Niger, kaskazini mwa Abuja, mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

342/